AMF yakabidhi vitabu 1,104 Pemba

09Apr 2023
Maulid Mmbaga
Nipashe Jumapili
AMF yakabidhi vitabu 1,104 Pemba

TAASISI ya Asma Mwinyi Foundation (AMF) imekabidhi vitabu vya elimu ya dini (juzuu) 1,104 kwa wanafunzi wa madrasa ya Shifaiya Islamiyya iliyopo Kinyasini Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni muendelezo wa sadaka wakati wa ibada ya mfungo wa Ramadhani.

AMF ambayo inajishughulisha na kuwasaidia wenye mahitaji maalumu hasa wanawake, wazee, watoto na walemavu, imekuwa pia ikitoa misaada mbalimbali katika nyumba za ibada, hospitali na jamii kwa ujumla.

Akikabidhi msaada huo jana Zanzibar, Mjumbe wa taasisi hiyo Abdalla Amour, alisema wamekabidhi vitabu 1,104 katika madrasa hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 150 kwa lengo la kuendelea kurithisha elimu ya dini kwa watoto na jamii ambayo itasaidia kudumisha utulivu katika nyanja mbalimbali.

“Urithi pekee kwa vijana wetu ni elimu ya dunia na dini, hivyo ni vyema wote kwa ujumla kushikamana na kuhakikisha jamii na watoto wanakuwa katika maadili mazuri ya kumjua Mungu, kwani hiyo itasaidia katika kupunguza mmomonyoko wa maadili kwenye jamii zetu,” alisema Amour.

Mwalimu Mkuu wa Madarasa hiyo Salama Juma Haji, aliishukuru Asma Mwinyi Foundation kwa kuwapatia vitabu hivyo, huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuiga mfano huo katika kujitolea kuisaidia jamii.