Imedaiwa na majirani kuwa huenda Bwanga ambaye ni maarufu mjini hapa, amefikia hatua hiyo ya kukatisha uhai kutokana na msongo wa mawazo baada ya kukimbiwa na mke na watoto.
Diwani wa Nyamisangura, Thobias Ghati, na mwenyekiti wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye, walieleza kusikitishwa na kifo cha Bwanga ambaye alikuwa maarufu mjini hapa.
“Tumesikitishwa na kifo cha kujinyoga cha mkazi wa mtaa wetu huu wa Ronsoti. Inawezekana huenda alikumbwa na msongo wa mawazo baada ya kukimbiwa na mke pamoja na watoto na kwenda kuishi mbali na yeye na kubaki mwenyewe.
Kifo hiki kimeleta majonzi katika mtaa wao na kata ya Nyamisangura. Tunatoa wito kwa jamii wanapokuwa na migogoro ya kifamilia, wajaribu kuwashirikishandugu wa karibu na viongozi wa serikali ili kutatua na kuishi kwa amani, kutunza familia kwa ajili ya maendeleo ya familia na taifa badala ya kujichukulia sheria mkononi ikiwamo uamuzi mgumu kama wa kujitoa uhai. Jambo hili kwa Mwenyezi Mungu halikubaliki,” alisema.
Kiboye, maarufu kama Namba Tatu, alisema: “Tunasikitika sana wakazi wa Ronsoti kwa tukio hili la Bwanga kujinyonga nyumbani kwake. Mbali na kukimbiwa na mke na watoto, asingechukua uamuzi mgumu wa kujitoa uhai kwani wanawake kutoroka na kwenda na watoto si jambo geni.
“Nadhani suala hili lingeweza kusuluhishwa na kurejea pamoja na kuishi kama kawaida na familia yake.Hili la kujitoa uhai ni kitendo ambacho kinatakiwa kulaaniwa na jamii kujiepusha na kujichukulia sheria mkononi.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime Rorya, Kamishna Msaidizi (ACP) Michael Njera, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi na kujitoa uhai.
Aidha, alitoa wito kwa jamii kama kuna mgogoro wa kifamilia, ni bora kufikisha kwa ndugu na jamaa wa karibu na hata uongozi wa serikali ili kusuluhisha badala ya kujitoa uhai.
Kamanda Njera alisema mwili wa Bwanga umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Wilaya Tarime kwa uchuguzi zaidi.










