Katika taarifa yake iliyosomwa jana na Ofisa Mawasiliano wa serikali ya Mkoa huo, Jeremia Mwakyoma, Rugimbana alisema kama itabainika kwamba kulikuwa na uzembe kwenye tukio hilo basi askari hao watachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Ni siku sita sasa zimepita baada ya Rais John Magufuli kuelezea kushangazwa kwake na askari polisi kunyang’anywa silaha na majambazi wakati wenyewe wana silaha.
Watu saba wanaosadikiwa kuwa majambazi wawapora askari silaha hiyo juzi usiku baada ya kuvamia ofisi za kampuni ya simu za mikononi ya Halotel katika eneo la Medelii Manispaa ya Dodoma na kuwajeruhi askari polisi waliokuwa zamu kwa nondo.
“Ni aibu kumuona askari Polisi mwenye silaha ananyang’anywa silaha, ni aibu, na nasema hiyo ni aibu, mpaka jambazi akunyang’anye silaha na wewe una silaha?” kauli ya Rais John Magufuli aliyoitoa siku sita zilizopita alipokuwa akihakiki silaha zake.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa hapa, David Mnyambuga, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Machi 25, mwaka huu majira ya saa nane na nusu usiku katika ofisi hizo.
Aidha, alisema katika tukio hilo baadhi ya askari walipatwa na majeraha madogo ambapo walitibiwa na kuruhusiwa huku Askari aliyefahamika kwa jina la Shadrack akijeruhiwa kichwani na kulazwa katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma na aliruhusiwa baada ya afya yake kuimarika.
Rekodi za matukio ya polisi kuporwa silaha na majambazi zinaonyesha kuwa Julai 12, mwaka 2015 majambazi waliwapora silaha aina ya SMG 15 na risasi askari polisi wa kituo cha Stakishari jijini Dar es Salaam na Septemba 7, 2010 majambazi yalivamia kituo cha polisi Bukombe SMG 10.
Katika tukio lingile lililotokea Kongowe Machi 30, 2015, majambazi yaliwapora askari SMG 2 na risasi wakati katika uvamizi wa kituo cha Kilombero, Februari 3, 2015, waliwapora askari SMG 1 na risasi 30 .
Katika uvamizi wa majambazi uliofanyika katika kituo cha polisi Mkuranga Juni 12, 2014, walifanikiwa kupora bunduki tano na risasi 60 huku katika kituo cha polisi Geita kweney uvamizi uliofanyika Februari 3, mwaka 2015 walipora SMG 10 na walipovamia kituo cha polisi Ikwiriri walipora bunduki tano na risasi 60.










