Ajali yaua wanane, yajeruhi sita Kigoma

24Dec 2023
Na Mwandishi Wetu
Kigoma
Nipashe Jumapili
Ajali yaua wanane, yajeruhi sita Kigoma

WATU wanane wamefariki dunia akiwemo mtoto wa umri wa mwaka mmoja na nusu na wengine sita kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha gari aina ya Toyota Probox iliyogongana na gari ya kampuni ya ujenzi ya Barabara ya Chiko katika eneo la barabara ya Kibondo-Kakonko mkoani Kigoma, ambapo chanzo cha-

-ajili hiyo kimetajwa kuwa ni uzembe wa dereva wa dereva wa gari ndogo Pamoja na mwendokasi.

Akizungumza leo Desemba 24, 2023 na waandishi wa habari kuhusiana na ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema ajali hiyo imetokea jana Jumamosi majira ya saa 11:30 jioni katika Kijiji cha Mumkungwa, Kata ya Misenzero, Barabara ya Kibondo-Kakonko.

Andengenye amesema majeruhi hao wapo katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwaajili ya matibabu na baada ya uchunguzi majeruhi watatu kati ya sita waliopata ajali wameumia zaidi hivyo watapewa rufaa kwenda Hospitali ya Bugando iliyopo mkoani Mwanza na wengine watatu wanaendelea na matibabu hospitalini hapo.

Waliofariki kwenye ajali hiyo wametajwa kuwa ni Pamoja na dereva wa gari ndogo, Hamisi Chaurembo (27), Bernadina Reuben (22), Madua Asukile, Ntiganiza Bihezako (67), Vedastus Paul (28), Vladmir Vedastus (1) marehemu wengine wawili ambao majina yao hayajatambuliwa hadi sasa.

Waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo wametajwa kuwa ni dereva wa gari la CHICCO, Flavian Felishian (28) aliyejeruhiwa kichwani na kifuani, Juma Saidi (27), Daniel Samwel (33), Silvanus Muhigwa (43) Sara Bundala na Dori Mafumbo (22).

Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu ambaye alitembelea eneo la tukio alitaja gari zilizohusika na ajali hiyo kuwa ni T 833 DUA aina ya FAW mali ya kampuni ya CHICCO na gari ndogo aina ya Toyota SUCEED yenye namba za usajili T 890 DYZ mali ya Hamisi Chaurembo dereva wa gari aliyefariki kwenye ajali hiyo.

Kamanda Makungu amesema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa dereva wa gari ndogo na ambaye alishindwa kulimudu gari hilo kwenye kona kali hivyo kugongana uso kwa uso na gari hilo la CHICCO.