Akizungumzia tukio hilo, baadhi ya wananchi akiwamo Salomon Nkini, alisema kutokana na kukithiri kwa tembo hao katika maeneo ya mashamba na kufanya uharibifu, walilazimika kuweka ulinzi ili kunusuru hasara.
“Usiku wa kuamkia Agost 8, mwaka huu, nilipigiwa simu na walinzi wengine waliokuwa wanalinda shamba langu kwamba kuna mlinzi amepoteza maisha baada ya kushambuliwa na tembo. Nilifanya jitihada za kwenda shambani na kuwasaidia waliobaki pamoja na kuongeza nguvu za kuwafukuza waliobaki,” alisema.
Alisema kundi la tembo kutoka msitu wa asili wa Kilimanjaro liliingia kwenye mashamba ya wakulima eneo la Pongo na walinzi walichukua jukumu la kupiga kelele za kuwafukuza na walionyesha dalili za kuondoka, ghafla mmoja aliyekuwa na mtoto aligeuka nyuma na kuanza kuwafukuza.
“Mara baada ya tembo huyo mwenye mtoto kuanza kuwakimbiza, marehemu aliishiwa nguvu na kuanguka ambapo tembo huyo alimshambulia nakisha kuondoka zake,” alisema Nkini.
Naye Maria Ndosi, alisema tembo hao wameendelea kuwa tatizo hasa nyakati za kuvuna na kuiomba serikali kuongeza nguvu ya kuwafukuza ili kuepusha madhara yatakayoweza kujitokeza yakiwemo ya watu kupoteza maisha pamoja na tatizo la njaa.
“Kwa sasa hakuna kulala, makundi ya tembo yamekuwa yakishuka kwa wingi na kufanya uharibifu mkubwa bila fidia yoyote. Tunaomba serikali kuongeza wataalamu katika kuhakikisha wanawafukuza wanyama hao pamoja na kulipa fidia kwa wakulima wanaopata hasara kutoka na wanayama hao, “alisema Ndosi.
Elisante Mfoi alisema hasara na vifo vitokananyo na wanyama hao vinachangiwa pia na maofisa wanyapori kuchelewa kuwajibika mara wanapopewa taarifa juu ya uwepo wa makundi hayo ya tembo kwenye mazao jambo ambalo wananchi wanaamua kuingia na kuanza kufanya kazi wenyewe.









