30 wavamia kituo cha polisi

21Feb 2016
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe Jumapili
30 wavamia kituo cha polisi

KUNDI la watu wanaokadiriwa kuwa 30 wakiwa na silaha za jadi, lilivamia kituo cha polisi Duthumi kilichopo tarafa ya Bwakila, Wilaya ya Morogoro na kuvunja mlango wa mkuu wa kituo hicho kwa lengo la kuwatoa wenzao watatu wanaotuhumiwa kwa wizi wa mifugo.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Graifton Mushi.

Katika tukio hilo lililotokea juzi, jioni Polisi walilazimika kutumia risasi na mabomu ya machozi kuwatawanya watu hao ambao kati yao watatu walijeruhiwa.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Graifton Mushi alisema watu hao walikuwa na mapanga, mashoka na marungu.

Alisema walivamia kituo hicho na kutaka kuwatoa wenzao ambao wanatuhumiwa kwa wizi wa ng’ombe sita, mbuzi wanne na kondoo mmoja mali ya Teu Saningo ambaye ni mfugaji wa jamii ya kimasai na mkazi wa kijiji cha Bwakila Chini.

Mushi alisema wakati watu hao wanavamia kituo hicho, watuhumiwa hao walishaondolewa kituoni hapo na kupelekwa katika kituo cha polisi kati Morogoro.

Kufuatia tukio hilo, polisi walifanya msako na kufanikiwa kuwakamata watu watatu kwa tuhuma za kuhusika na uvamizi huo.

Alisema watafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Katika tukio jingine, zaidi ya wananchi 20 wa kitongoji cha Mazizini kijiji cha Maseye Wilaya ya Morogoro, walivamia eneo la mwekezaji Ayubu Mngimbwa anayefanya shughuli za kuchimba madini na kuteketeza vibanda vilivyokuwa na vifaa mbalimbali vya kuchimbia madini.

Mbali na kuteketeza vifaa hivyo, watu hao walimvamia na kumshambulia kwa kipigo mwekezaji huyo na baada ya kuokolewa alipelekwa katika hospitali ya rufaa Morogoro na kupatiwa matibabu kisha kuruhusiwa.

Kaimu Kamanda huyo alisema kuwa thamani ya vibanda na vifaa vilivyoteketezwa bado haijafahamika na chanzo cha tukio hilo ni mgogoro kati ya wananchi wa kitongoji hicho na mwekezaji huyo anayedaiwa kutiririsha maji yenye kemikali za sumu wakati wa kusafisha madini yake.

Sumu hiyo inadaiwa kuingia kwenye mto unaotumiwa na wananchi.
Kufuatia tukio hilo, mtuhumiwa mmoja ambaye ni mfanyabiashra wa Maseyu amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuwaongoza watu kwenda kumvamia mwekezaji huyo na atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.