1000 waboreshewa maisha Babati

23Apr 2023
Jenifer Gilla
Nipashe Jumapili
1000 waboreshewa maisha Babati

WAKAZI takribani 1000 kutoka vijiji 10 vinavyozunguka mapitio ya wanyama ya Kwakuchinja wameboreshewa maisha kupitia mradi wa Mkono kwa Mkono wenye lengo la kuziinua jamii hizo kiuchumi ili kuachana na ujangili wa wanyamapori.

Meneja wa mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya utalii ya Chem Chem, Nganashe Lukumay, alisema mpaka sasa wameshatoa fedha kwa  vikundi 55 vya vikoba, Sh. milioni moja hadi milioni mbili kutegemea na malengo ya kikundi, ambazo wanazitumia kuanzisha biashara ya pamoja  kukopeshana ili kupata fedha za mitaji.

Alisema pia wanawapatia mafunzo yatakayowasaidia kuongeza thamani katika shughuli zao wanazozifanya ikiwamo kunenepesha mifugo, elimu ya biashara, ufugaji wa kuku, nyuki, kilimo cha mboga za majani na  alizeti.

Nganashe alisema  lengo la mradi huo ni kuziwezesha jamii  zipate njia mbadala ya kujiongezea kipato tofauti na kutegemea kwenye mali asili kama vile msitu na wanyama hali inayochangia kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na viumbe hao.

Alisema tangu kuanzishwa mradi huo miaka sita iliyopita  wamepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wanakijiji ambao wameunda vikundi vya vikoba vyenye asilimia 80 kinamama ambao huongezewa pesa kwa ajili ya kufanya biashara au kukopeshana ili kufanya shughuli binafsi za kiuchumi.

“Tunawapa mtaji kama kikundi kwa ajili ya kuwekeza au kukopeshana ili kila mwanakikundi aanzishe biashara, mwisho wa mwaka wakishavunja kikundi watagawana faida iliyopatikana katika miradi yao na ile fedha tuliowapa inabaki kwenye mfuko kwa ajili ya kuanzia mwaka unaofuata, njia hii imepunguza sana ujangili,” alisema.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Upendo, kilichopo Kijiji cha Vilimaviwili Flora Godson, alisema kupitia mradi huo walipata mkopo wa Sh. milioni mbili ambazo walizikopesha kwa wanakikundi ili kupata fedha za mitaji ya biashara ndogo.

Alisema mikopo hiyo imesaidia wanawake wa kikundi hicho kuwa na sauti katika familia zao kwa kuwa sasa wanawasaidia waume zako kuendesha familia kwa  fedha zinazotokana na biashara wanazofanya jambo ambalo huko nyuma halikuwapo.

“Sasa hivi hata waume zetu wamepunguza ukali na kutuona hatuna thamani kwa kuwa na sisi tunaweka fedha mezani, zamani ilikuwa ukitoa ushauri kwa muwe wako anakuangalia tu kisha anakupuuzia, kwa kweli tunawashukuru Chem Chem kwa kutuinua wanawake,” alisema.

Mwanachama wa kikundi hicho, Glosary Mgahawe, alisema mafunzo ya ujasiriamali aliyopata kupitia mradi huo yanamsaidia katika uendeshaji wa biashara yake ya mgahawa na sasa anaweza kurudisha mkopo wa vikoba kwa wakati tofauti na awali.

“Kabla ya mafunzo nilikuwa sina nidhamu ya fedha, hela nilikuwa nazitumia ovyo bila kuandika kwenye daftari matokeo yake ikifika mwisho wa wiki nakosa hela za marejesho mwisho wa mwaka nafilisiwa na kukosa faida, lakini mafunzo haya yameniweka kwenye mstari nashukuru Mungu,” alisema Glosary.