Demu ananipenda, lakini kwa wazazi hataki kwenda!

04Jan 2016
Flora Wingia
Nipashe
Demu ananipenda, lakini kwa wazazi hataki kwenda!

Mpenzi msomaji, HERI ya MWAKA MPYA! Naamini kwa kudra za Mwenyezi Mungu umeuona mwaka mpya wa 2016. Tuendelee kumshukuru Mungu kwani yeye ndiye aliyeubeba uhai wetu. Tumhimidi na tumpe sifa zote kwani anastahili.

Naam.Makala yetu ya mwisho mwaka jana tulijadili kwamba zipo roho zinazotenganisha marafiki, wanandoa. Tukaangalia mifano miwili jamaa aliachana na mkewe mwaka mmoja, lakini mawasiliano yakiwa bado yanaendelea.

Mwanaume anamsihi mkewe arudi na mke naye anamwambia japokuwa anaishi na mwanaume mwingine, eti huyu ajipange atamrudia.

Kijana yuko njia panda. Hapa kipo kitu kilivuruga mahusiano haya hata kutengana. Hiyo ni roho yaweza kuwa ni marafiki, majirani, wazazi wa mmojawapo au wawili hao walikuwa na matatizo yaliyofanya mahusiano yavunjike.

Mwingine ni msichana ambaye kila kijana ampatae japokuwa wanapendana, lakini baada ya muda wanaachana. Walifikia wavulana watatu wakiachana katika mazingira yasiyoeleweka.

Hapo lazima kipo kitu. Wapo wafitini wanaosababisha mifarakano ya wengine.

Leo hebu wasikie na hawa kupitia ujumbe wao mfupi simu ya kiganjani.
…Naipenda sana safu ya Maisha Ndivyo Yalivyo.

Dada naomba ushauri mimi sijaoa lakini nina demu (msichana) ambaye ninampenda na nilishamwambia kuwa niko tayari kumuoa.

Lakini kila nikimwambia twende nyumbani kwa wazazi wangu ananipiga chenga na wakati mwingine anatoa sababu. Je, dada huyu ananipenda kweli? (Amani wa Dar). 07175471985

Mpenzi msomaji wangu, baada ya ujumbe huu nilimpa ushauri ufuatao;- hakupendi huyo, tuliza akili muombe Mungu atakuchagulia mwingine. Tatizo lenu mnaona dalili lakini unakuwa king’ang’anizi. Wanawake ni wengi papara za nini? Asante.

Sikuishia hapo. Kabla hajanijibu nikamuuliza tena; hivi, wote mmeshamaliza masomo au mnafanya nini? Na mna umri gani?

Ukomavu kiumri pia ni kigezo muhimu kwa wale wanaopanga kutambulishana kwa wazazi. Kijana huyu akarudisha ujumbe wa majibu akasema;-

“Asante dada Flora kwa jibu zuri. Kuhusu elimu wote tumehitimu elimu ya msingi.

Umri mimi nina miaka 31 na huyu demu umri miaka 28 wote ni wajasiriamali. Pia ninamshukuru Mungu kwani binafsi nimefanikiwa kununua kiwanja ingawa bado sijajenga.

Nilimshauri atulie, atafute hela ajenge nyumba yake na kwamba Mungu atamuonyesha mke wa kuoa.

Naye akajibu: “Poa shangazi nashukuru kwa ushauri wako.” Hivi ndivyo tulivyomalizana na kijana huyu na naamini maoni na ushauri wangu umemjengea matumaini mapya katika safari yake ya maisha anayoipigania.

….Mwingine ana malalamiko yanayofanana na hayo kama ifuatavyo;- …Mimi ni kijana umri mkiaka 24 ninakaa Tegeta. Kuna binti mmoja anaitwa Rahma ni jirani yetu nampenda sana. Ila nikimwambia hataki.

Nikimuomba namba ya simu hataki. Halafu akiniona anakuwa hacheki ila anawaambia wadogo zangu kwamba ananipenda. Sasa sijui kwanini hata nifanyeje naomba ushauri( naitwa Kim Doung Jin). 0715066696
Nikamuuliza; mbona jina la kichina? Na wote nyie wa wawili mna umri gani? Akanijibu; Nina miaka 24, ndio mimi ni Mkorea upande wa mama na rafiki huyu ana umri wa miaka 26.

Mpenzi msomaji, bila shaka umewasikia vema vijana hao. Huyo wa kwanza tatizo nilionalo hapo japokuwa wanapendana, lakini kuna aina fulani ya kutunishiana misuli. Kiumri wako vizuri. Kingine wote ni wajasiriamali.

Kijana yuko tayari hata kwenda kumtambulisha bibie kwa wazazi wake, lakini inaonyesha bibie huyu hayuko tayari kuingia kwenye mkataba wa ndoa.

Binafsi najaribu kuwaza tu, kwamba pengine bibie anaona biashara inakwenda vema na anaweza kujisimamia katika kujijenga kimaisha kabla hajaingia kwenye mikataba ya ndoa.

Anaona fedha zinaingia na hakuna bughudha. Sasa akiwaza kumilikiwa kama mke anasita. Wapo kinamama nimeona baada ya kujua mbinu za kujiinua kiuchumi, hawana mpango na wanaume.

Hawa ndio wale wanaoamua kujenga hata nyumba wenyewe kwa kipato chao, na kisha kuamua kutafuta mwanaume wa kuzaa nae bila masharti.

Kijana aliyetuma ujumbe nimemshauri hapo juu kwamba akiona bibie haelekei, basi atulizane ajenge nyumba yake na kisha taratibu atafute mwingine. Nikamshauri pia amuombe Mungu atamwonyesha mke mwema wa kuoa. Mithali 19: 14 …Bali mke mwenye busara mtu hupewa na BWANA.

Tukirejea kwenye ujumbe wa kijana wa pili, ni kwamba hawa bado wanaogopana. Msichana japokuwa anaonyesha kumpenda lakini bado anasita. Inawezekana ni kutokana na kwamba ni Mkorea wenzake wanamshuta au bado hayuko tayari kwa mahusiano.

Kijana yeye anaonyesha japokuwa anapenda lakini ujasiri wa kukabiliana na msichana wake huyo unakuwa hafifu anaishia kulalamika. Kumbe alipaswa kuonyesha ujasiri na uthubutu wa kuwa karibu na msichana huyo ili aweze kumweleza upendo wake kwake.

Mpenzi msomaji, Maisha Ndivyo Yalivyo. Hakuna aliyempata mke au mume kirahisi. Wengi wamepitia mitego mingi lakini mwisho wa siku wakafanikiwa au wakapoteza.

Ndiyo maana yatupasa wakati wote kumshirikisha Mungu katika kila tulifanyalo kwani yeye ni kila kitu.

Katika maandiko yake Mungu anasema; Mithali 16:1 Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa BWANA.

Niishie hapa, nini ushauri wako? Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]