CUF yapangua hoja za CCM kurudiwa uchaguzi Z'bar

31Dec 2015
Nipashe
CUF yapangua hoja za CCM kurudiwa uchaguzi Z'bar

Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kikiwataka wanachama wake kujitayarisha na uchaguzi mkuu wa marudio, Chama cha Wananchi (CUF), kimesema hakuna makubaliano yaliyofikiwa ya kurudiwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar na kuwataka wanachama wake kuendelea kusubiri maamuzi yatakayotolewa na Kamati ya Mazungumzo inayoongozwa na Mwenyekiti Rais wa Dk. Ali Mohamed Shein.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu.

Tamko hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo eneo la Vuga, Mkoa wa Mjini Magharib na kuzungumzia mkwamo wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

Jussa alisema mazungumzo ya kutafuta muafaka yanaendelea kufanyika na kuwakutanisha viongozi wa kitaifa wakiwamo Marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao ni Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Amani Abed Karume na Dk. Salmin Amour Juma.

Alisema kitakachoamuliwa na kamati ya mazungumzo ambayo wajumbe wake wengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, ndicho kitakachotoa hatma ya mkwamo wa uchaguzi wa Zanzibar.

Alisema taarifa iliyotolewa na CCM ya kuwataka wanachama wake wajitayarishe kwa uchaguzi wa marudio haina msingi na ukweli juu ya kinachoendelea kutokana na kuwa na kauli mbili zinazogongana, ya kuwataka wanachama wajiandae na uchaguzi na kuridhishwa na mazungumzo yanayoendelea Ikulu Zanzibar, wakati maazimio ya kikao hicho bado hayajatolewa.

Alisema Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CUF ililazimika kukutana Desemba 27, mwaka huu na kujadili kwa kina kauli ya CCM na kuamua kutoka na maazimio matano ikiwamo kuwataka wanachama wapuuze taarifa ya Katibu wa Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu, huku ikiwataka wanachama wake wajipange kwa uchaguzi wa marejeo.

Aidha, Jussa aliwataka wanachama wa CUF kumpa nafasi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kuendelea na juhudi za ngazi ya juu za kuhimiza upatikanaji wa ufumbuzi wa haraka juu ya mkwamo wa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.

“CUF haitatetereka, na itasimamia kwa dhati maamuzi yao waliyoyafanya Wazanzibari kwa njia ya kidemokrasia kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 na italinda chaguo lao la Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani wao,” alisema Ismail Jussa.

Alisema wakati macho na masikio ya wananchi yametega Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Wazanzibari wanastahili kupongezwa kwa kuonyesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa kwa kuendelea kutunza amani na utulivu wakati viongozi wa kitaifa wakiendelea na mazungumzo ya kutafuta muafaka wa kutanzua mkwamo huo.