Wizara yaanza kupima afya udongo kubaini mbolea kutumika shambani

16Jul 2022
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Wizara yaanza kupima afya udongo kubaini mbolea kutumika shambani

WIZARA ya Kilimo imeanza kupima afya ya udongo nchi nzima ili kuwasaidia wakulima kutambua mazao gani walime na aina ipi ya mbolea watumie ili kilimo chao kiwe na tija.

Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde, alibainisha hayo jana alipokuwa akizungumza na wakulima wa kata ya Hombolo, jijini Dodoma baada ya kutembelea na kukagua mashamba darasa yaliyotumia mbolea zinazozalishwa na kiwanda kipya cha Mbolea cha Itracom.

“Kazi hii ya upimaji udongo itatusaidia pia kuwa na kanda za kilimo ili mazao yalimwe kwa kanda siyo kila mkulima kujipandia mazao ambayo yeye anaona yanamfurahisha ili kusadia pia wakulima kuacha kulima kilimo cha kubahatisha,” alisema Mavunde.

Pia aliwataka wakulima wote nchini kuzingatia matumizi ya mbolea katika kilimo chao ili kiwe na tija tofauti na ilivyo sasa ambapo wanawekeza nguvu nyingi lakini tija ni kidogo sana.

“Matumizi ya mbolea katika kilimo hivi sasa hayakwepeki kama mkulima anataka kupata tija tuachane kabisa na dhana ya kuwa kutumia mbolea unaharibu ardhi,” alisema Mavunde.

Kadhalika, alisema kupitia kilimo nchi itakuwa na uhakika wa chakula, ajira, kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla.

“Katika bajeti ya mwaka huu kwenye kilimo, kila sekta imeongezewa kiasi kikubwa cha fedha ikiwemo katika utafiti na umwagiliaji. Niwaombe watafiti mnapofanya utafiti wenu hakikisheni matokeo yanawafikia wakulima mapema ili wapate mbinu bora za kilimo na kuongeza tija,” alisema.

Pia alisema serikali inapanga kufufua mabonde yote ambayo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji ili kusaidia wakulima kulima kwa kipindi chote cha mwaka.

“Lazima tuwekeze katika sekta hii ya kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili mvua zinapo kuwa chache kama mwaka huu tunakua na uhakika wa chakula kwa kutumia umwagiliaji,” alisisitiza Mavunde.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk. Stefan Ngaito, aliwatoa hofu wakulima kuhusu matumizi ya mbolea.

Alisema wamekuwa wakipima na kuthibitisha ubora wa mbolea zote za ndani na nje ya nchi.

“Niwasihi wakulima nchini kuhakikisha kuwa wanatumia mbolea katika kilimo chao kwani sisi tumekuwa tukipima mbolea zote na hii inayozalishwa na kiwanda hiki cha Itracom tumeipima na kuidhinisha kuwa inafaa kwa matumizi ya wakulima wetu na itawapa tija katika kilimo chao,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Itracom, Nduwimana Nazaire, alisema wamepanga kuanza uzalishaji wa mbolea mwishoni mwa mwezi huu.

Nazaire alisema mwishoni mwa mwezi huu wataanza uzalishaji wa tani 200,000 za mbolea na mwakani watazalisha tani 600,000.

“Mbolea yetu tunayozalisha ni rafiki wa udongo kwani inaongeza virutubisho na kurejesha rutuba lakini pia kutokana na kutumia malighafi za hapa nchini bei yake itakuwa chini sana ukilinganisha na zile zinatoka nje ya nchi,”alisema.