Watanzania changamkieni fursa za kibiashara EAC - Mahiga

01Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Watanzania changamkieni fursa za kibiashara EAC - Mahiga

WATANZANIA wametakiwa kuchangamkia fursa za kibiashara zinazoletwa na Mtangamano wa Afrika Mashariki, kwani ushirikiano wa mataifa ndiyo njia pekee ya kuleta maendeleo ya nchi kwa pamoja.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga

Wito huo ulitolewa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi, Dk. Augustine Mahiga, wakati wa uzinduzi wa kituo cha kwanza cha mpaka wa pamoja kati ya nchi za Tanzania na Kenya, kiitwacho One Stop Border Post (OSBP), katika mpaka wa Holili mkoani Kilimanjaro.

Kituo hicho cha ushuru wa pamoja kimegharimu Dola milioni 12 za Marekani zilizotolewa na Taasisi ya TradeMark East Africa (TMEA).

Balozi Dk. Mahiga aliyemwakilisha Rais Rais John Magufuli, alisema ushirikiano wa kimataifa ndiyo njia pekee ya kuziwezesha nchi kujiletea maendeleo na kutoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa zinazoletwa na uwapo wa kituo hicho.

Naye Waziri wa Kazi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Kenya, Phyllis Kandie, elisema kituo hicho kitaongeza fursa za kibiashara zaidi kati ya Kenya na Tanzania.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Balozi. Dk. Richard Sezibera, alisema uzinduzi wa kituo hicho ni moja ya vituo nane vya mipakani vilivyokamilika vikisubiri uzinduzi.

Mwakilishi wa Taasisi ya TMEA, Theo Lyimo, ambaye ni Mkurugenzi wa vituo hivyo vya OSBPs wa TMEA, aliwashukuru wafadhili - DFID, Canada, Usaid na Benki ya Dunia kwa kutoa fedha kufadhili mradi huo na kazi iliyobakia kwa vituo hivyo ni kuunganishwa kwa njia ya mtandao na taasisi nyingine zote.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na mawaziri, mabalozi, wakuu wa taasisi mbalimbali, wabunge na wananchi wa kawaida wa nchi za Tanzania na Kenya.