Inaelezwa kuwa matumizi ya nembo (logo) ambayo tayari imesajiliwa na mtu mwingine ni kinyume cha sheria na mtumiaji akibainika bidhaa hizo zinaweza zikataifishwa, kuteketezwa pamoja na kumlipa fidia mmiliki wa nembo husika.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Sheria kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Kelvin James wakati wa utolewaji wa elimu ya miliki buninifu kwa Wafanyabiashara wadogo na wakubwa mkoani Mwanza na kuwataka ambao bado hawajasajili nembo zao kufanya hivyo.
“Tunawasisitiza na kuwashauri wafanyabiashara na wajasiliamali wote kuhakikisha wanasajili nembo za kampuni zao kupititia Brela Kurugenzi ya miliki bunifu ili kulinda na kupata hati za udhibitisho juu ya umiliki wa nembo zao,” amesema James
Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Hataza kutoka Kurugenzi ya miliki bunifu Brela, Neema Kitala amesema kuwa wameanza kuzunguka kila wilaya wakianza na Mkoa wa Mwanza kutoa mafunzo kwa wafanyara lengo likiwa ni kuwasaidia kulasimisha miliki bunifu zao.
Aidha, ameongeza kuwa wafanyabiashara wengi hawana uelewa juu ya miliki bunifu hivyo kuamua kuwafuata katika maeneo yao ili kuwasaidia kusajili biashara zao ili kuwa na ulinzi kisheria.
Mmoja wa wafanyabiashra hao, Wilhelmina Kubingwa ameiomba serikali kupitia Brela kuhakikisha wanatoa elimu juu ya miliki bunifu kwa mawakala wao ngazi za mikoa ili kuondoa usumbufu wa kucheleweshwa katika ufuatiliaji wa usajili.










