Wafanyabiashara wachungulia fursa kwenye dawa za asili

15Nov 2023
Beatrice Moses
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wafanyabiashara wachungulia fursa kwenye dawa za asili

Hatua ya serikali kuruhusu rasmi dawa za asili kuingia kwenye mfumo wa tiba katika hospitali za umma, imetajwa kuwavutia wafanyabiashara kadhaa, ambapo baadhi yao wamejiunga kwenye kozi fupi zinazotolewa na Taasisi ya Tiba Asili ya Muhimbili. 

Mhadhiri na Mshauri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili(MUHAS)DK. Mourice Mbunde amesema hatua  ya wafanyabiashara hao inachochewa na kuona fursa ya kibiashara kwenye dawa hizo ambazo hadi sasa zilizosajiliwa ni 102. 

Dk. Mbunde ameyasema hayo katika mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu tiba za asili zilivyotumika katika janga la COVID-19.Amesema tiba hizo zilionyesha matokeo mazuri, ambayo yalithibitishwa na tafiti mbili tofauti zilizofanywa katika kubaini usalama wa dawa hizo. 

Katika mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania(TAMWA) Dk. Mbunde amesema dawa hizo zilizoruhusiwa na serikali baadhi zitibu magojwa ya matatizo ya kupumua pia  magonjwa 14 yasiyoambukiza na magonjwa 7 ya kuambukiza. 

Magonjwa yaliyotajwa kutibiwa na dawa hizo asili  ni pamoja na shinikizo la juu la damu, kisukari malaria, vidonda vya tumbo, UTI, pumu, uvimbe wa tezidume.

Mengine ni mgoro,sundo, mba wa ngozi na nywele bawasiri, kupoteza fahamu au kumbukumbu, usaha masikioni, mifupa kupauka na mafindofindo. 

Magonjwa mengine yanayotibiwa na dawa hizo za asili ni uvimbe tumbo la uzazi, maumivu ya meno na fizi,mba ukeni,maumivu ya tumbo wakati wa hedhi, maumivu ya maungio na mifupa, nguvu za kiume, kuharibika mimba mara kwa mara.

Dk.Mbunde amesema pia hatua hiyo ya serikali tayari imeonyesha kuwa ni fursa ya kiuchumi kwa kuwa MUHAS, sasa inapokea watu wa kada tofauti wakiwamo wafanyabiashara kujifunza kozi fupi wakiamini. 

Amina Ally kutoka asasi za kiraia amesema kuruhusiwa mwa dawa hizo ni faraja kubwa kwa kuwa ni dawa ambazo zimekuwa zikitumika na mababu na mabibi enzi hivyo ni kuendeleza utamaduni. 

Akizungumzia kwa niaba ya Mkurugenzi wa TAMWA, Florence Majani wakati akifungua mafunzo hayo ya siku moja amesema waandishi wanapaswa kuendeleza kujifunza mambo kadhaa kuhusu COVID kwa kuwa ni ugonjwa ambao unaaminika bado upo. 

Majani amesema, hivyo waandishi wa habari wanawajibika kufikisha taarifa sahihi kwa jamii ili kuepusha athari ikiwamo vifo.

Agosti 30,2023 Mkurugenzi  wa Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya Profesa Pascal Rugajo alizungumzia hatua hiyo ya serikali wakati akifungua kongamano la pili la kisayansi na Maonesho ya dawa za tiba asili, alisema Kwa kuanzia dawa 19 za asili ndizo zitapatikana kwenye Hospitali 7 za Kanda nchini.