Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Maendeleo kata ya Toangoma, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Masuliza, Aziz Mwinyimkuu, amesema uanzishwaji wa kikundi cha HOREG ni hatua kubwa katika kuwakomboa wanawake wa kata hiyo.
“Sisi viongozi wenu tunawaunga mkono, tunatambua thamani ya kazi mliyoianzisha. Nimeona mnahitaji vyerehani na vitu vingine ili kufikia malengo, niwaombe wadau wote wawaunge mkono ili safari ya kumwinua mwanamke kiuchumi ifanikiwe,” amesema.
Amezitaka taasisi na kampuni zikisaidie kikundi hicho kwa vifaa vya kazi ili wanawake na mabinti waweze kupata ujuzi stahiki.
Mwenyekiti wa HOREG, Fausta Ndunguru, amesema nia ya kuanzisha kikundi hicho ni kutoa ujuzi kwa wanawake ili wapate ajira zenye staha.
“Tunajua wanawake tuna uwezo wa kufanya mambo makubwa kama tukiamua. Niwaalike wote wenye uhitaji wa ujuzi waje wajifunze, zaidi sana nawaomba wadau wa maendeleo watushike mkono ili lengo la kumkomboa mwanamke kiuchumi litimie,” amesema.
“Nitumie fursa hii kuwatia moyo wanawake popote walipo kwamba wasikate tamaa lakini niwakumbushe kwamba ujuzi ni muhimu ili tuwe kwenye ajira za heshima,” amesema.