Viongozi wa Senet watoa elimu ya itikadi kwa wanachuo Kolandoto

19Nov 2023
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe Jumapili
Viongozi wa Senet watoa elimu ya itikadi kwa wanachuo Kolandoto

VIONGOZI wa Senet ya vyuo na vyuo vikuu Mkoa wa Shinyanga wa Umoja wa Vijana (UVCCM), wamefanya ziara katika Chuo Cha Sayansi za Afya Kolandoto katika Manispaa ya Shinyanga kwaajili ya kutoa elimu ya itikadi kwa wanachama wa senet pamoja na kuwapatia kadi za CCM.

Ziara hiyo imefanyika jana na kuongozwa na Mwenyekiti wa Senet, Said Sultani ambayo iliendana sambasamba na kuhamasisha kuongeza idadi ya wanachama wapya, ili kuendelea kukiimarisha Chama cha Mapinduzi (CCM) na Jumuiya zake.

Sultani akizungumza na Wanachama wa Senet katika chuo hicho cha Sanyansi za Afya Kolandoto, amesema katika Mkoa wa Shinyanga wana matawi 13 ya senet, pamoja na mambo mengine wamekuwa wakitoa elimu ya itikadi, imani ya CCM na ahadi tisa za CCM, ili kuwajenga vijana kuwa wazalendo na nchi yao.

Katika hatua nyingine Sultani amempongeza Rais Samia kwa kuridhia utoaji wa mikopo katika vyuo vya kati, hali ambayo itasaidia wanafunzi ambao kaya zao hazina uwezo wa kuwasomesha vyuo kupata fursa ya kusoma na kutimiza ndoto zao na hata kuja kuwa viongozi wa taifa hili.

"Desemba 02, mwaka huu tutaandaa Kongamano la ‘Asante Mama’ hapa mkoani Shinyanga na mgeni rasmi tunatarajia awe Katibu wa NEC, Itikadi, Siasa na Uenezi Paulo Makonda, sababu Rais wetu Samia amefanya mambo makubwa ya maendeleo ikiwamo sekta ya elimu," amesema Sultan.

Naye Mwenyekiti Mstaafu wa Senet kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Pius Mwandu, akitoa elimu ya itikadi kwa kuanza na imani ya CCM, amesema kuwa imani ya CCM ni kujenga ujamaa, kuishi kwa usawa na binadamu wote ni sawa.

Akizungumzia ahadi tisa za CCM ili kuwafanya vijana kuwa wazalendo na nchi yao, amesema zinaeleza kuwa binadamu ni ndugu wa Afrika Moja, kutumikia nchi kwa watu wote, kujitolea nafsi kuondosha umaskini, ujinga na dhuruma.

Ametaja zingine kuwa rushwa ni adui wa haki, cheo ni dhamana na kutokitumia kwa faida binafsi, kujitoa kwa elimu kwa faida ya watu wote, kushirikiana na watu wengine kujenga nchi, kusema ukweli fitina mwiko pamoja na kuwa mwanachama wa CCM na raia mwema.

Pia ametoa wito kwa viongozi wa Senet vyuoni kuyasema mambo mazuri ambayo yamefanywa na Rais Samia ya kuliletea maendeleo taifa katika sekta mbalimbali ikiwamo ya elimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Sanyansi za Afya Kolandoto Paschal Shiluka ambaye ndiye mlezi wa Senet Chuoni hapo, amepongeza ziara hiyo huku akisema kuwa wao kama vyuo vya mafunzo wanaunga juhudi za Rais Samia katika utendaji wake kazi na Chama Cha CCM sababu wao ndiyo wanaongoza nchi.