TTCL kugharamia watu 204 watakaopandisha bendera Mlima K'njaro

05Dec 2023
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
TTCL kugharamia watu 204 watakaopandisha bendera Mlima K'njaro

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limejitosa kubeba gharama za huduma zote za mawasiliano ya intaneti bure kwa wazalendo 204 watakaopandisha bendera ya taifa  katika kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro, kuelekea maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL nchini, John Yahaya, akifafanua jambo kuhusu kampeni ya twenzetu kileleni 2023.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, John Yahaya, akizingumza jana kabla ya wazalendo hao kuanza safari ya kupanda mlima huo, kupitia kampeni ya twenzetu kileleni 2023 amesema:

"Tukio hili linaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya nchi yetu, katika kukuza sekta ya utalii sambamba na kuimarisha mawasiliano nchini,"

Amesema, Shirika hilo limeendelea kutekeleza mkakati wake wa kuimarisha mawasiliano nchini kwa kuhakikisha kunakuwepo na miundo mbinu ya kisasa na yenye uwezo mkubwa katika kutoa huduma ndani na nje ya Tanzania.

Amesema katika safari itakayoanza kesho ya kupanda mlima Kilimanjaro, shirika hilo kwa kutambua umuhimu wake, itatoa huduma ya inateneti bure kwa washiriki watakaopanda mlima huo katika kipindi hiki cha kampeni ya twenzetu kileleni.

"Washiriki wote watakaopanda mlima Kilimanjaro, katika kipindi hiki cha kampeni ya twenzetu kileleni, watapata fursa hiyo ya intaneti bure wafikapo kila kituo katika mlima huo, ili kutambua umuhimu wa maadhimisho haya ya miaka 62 ya uhuru wa nchi yetu,"

Amesema uwepo wa huduma hiyo ya intaneti, itakuwa ni fursa ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika hifadhi ya mlima wetu, ndani na nje ya nchi yetu, lakini itahamasisha Watanzania kujenga mazoea ya kutembelea vivutio vya mlima Kilimanjaro na maeneo mengine ya utalii.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Shirika ka Hifadhi za Taifa (TANAPA), Jenerali Mstaafu, George Waitara, amewataka Watanzania kuendelea kuutangaza mlima huo kwa kutumia fursa mbalimbali zilizopo  hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanganyika.

"Utaratibu huu wa kupanda mlima wakati wa kusherekea uhuru wa nchi yetu, ulianza mwaka 2008 na sasa ni miaka 15 imepita, nafurahi kila mwaka mwitikio unakuwa ni mkubwa, na mwaka huu nimeambiwa tuko 200, hii ni hatua kubwa sana na watu wameitikia."

"Tusiachie watu wa nje kuja kututangazia mlima wetu, ni jukumu letu sisi wenyewe kuutangaza mlima huu, sisi wenyewe Watanzania tufanye kazi hiyo, sasahivi kumefanyika maboresho makubwa na huduma zote muhimu zinapatikana  kwa wanaopanda mlima Kilimanjaro na huduma za mawasiliano zimeboreshwa huko."

Aidha, wale wanaopanda mlima huo kuuheshimu na kwamba mlima siku zote hauzoeleki, ukiuheshimu nao unakuheshimu hivyo akawataka wale wanaopanda mlima huo kufuata maelekezo na taratibu zote wanazopewa kwa wale wanaowaelekeza.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Makampuni ya utalii ya  Zara Tours, Ibrahim Othman Jama, amesema watakaopanda mlima mwaka huu kutakuwepo na idadi ya watu 200 kutoka katika mashirika na taasisi mbalimbali.

"Tunalishukuru Shirika la TTCL kwa kutoa huduma za mawasiliano katika mlima Kilimanjaro, hii ni kazi kubwa ambayo imefanyika kwa kuwa itarahisisha huduma za mawasiliano kule mlimani, 

"Tunamshukuru Rais wetu,  Samia Suluhu Hassan kwa kupitia  filamu yake ya  'The Royal Tour' ambayo imeweza kuleta matunda mengi kwa kutangaza vivutio vyetu vilivyopo hapa nchini."