Tembo waharibu ekari 28 za mahindi

13Aug 2023
Cynthia Mwilolezi
SIMANJIRO
Nipashe Jumapili
Tembo waharibu ekari 28 za mahindi

WAKULIMA wa Kata ya Msitu wa Tembo, Simanjiro mkoani Manyara, wameharibiwa ekari 28 za mahindi, baada ya tembo kuvamia kwenye mashamba yao.

Diwani wa Msitu wa Tembo, Kaleiya Mollel, akizungumza jana kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika kwenye Mamlaka ya Mji Mdogo wa Orkesumet ameiomba serikali ichukue hatua.

Mollel alisema tembo hao wamevamia mashamba ya wananchi wa eneo hilo na kuharibu mazao, hivyo kusababisha wakulima kupata hasara ya ekari 28 za mahindi.

“Tembo hawatosheki hata ekari 500 haziwatoshi. Sasa ili kubakisha kile kilicholimwa tunaomba tembo hao waondolewe kwenye eneo la kata yetu,” alisema Mollel.

Pia alisema serikali inapaswa kuingilia kati suala hilo kwa kuwa wakulima watakumbwa na njaa kwa sababu ya kukosa mavuno.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Makota, alikiri kuwapo kwa tembo kwenye baadhi ya kata hiyo.

“Tuko kwenye mpango wa kumaliza kero na changamoto hiyo ya tembo kwa kuwafundisha wana vijiji namna ya kuwafukuza shambani tembo hao,” alisema Makota.

Naye Kaimu Ofisa Maliasili Halmashauri hiyo, Joseph Shamba, alisema wameandaa mpango wa kuwafundisha vijana wa maeneo husika ili wawafukuze tembo hao.

Shamba alisema kata zenye changamoto kubwa waandae vijana 10 au 30 kwenye vijijini, ili watengeneze mabomu kupitia fataki na tochi zenye mwanga mkali.

“Tunaanza na Kata za Msitu wa Tembo, Loiborsoit, Ngorika na Edonyongijape kwa kuwa ndizo zimeathirika mno, kisha maeneo mengine yatafuata”, alisema Shamba.