Meneja wa TANROADS mkoani humo, Regnald Masawe, amesema jijini hapo kuwa wananchi waliovamia na kujenga vibanda ndani ya hifadhi ya barabara, ndiyo watakaoathirika kwa kuwa hawana uhalali na eneo hilo na wanapaswa kuondoka mara moja.
Massawe alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki na wananchi wa Kisongo wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo iliyoibua taharuki kwa wafanyabiashara wadogo wa Arusha.
"Tupo hapa kwa ajili ya kuondoa vibanda, wananchi wanapaswa kuelewa kwamba yeyote aliyejenga kibanda ndani ya eneo la mita 30 kutoka katikati ya barabara ametenda kosa na anapaswa kuchukuliwa hatua na leo tumeanza kuviondoa vibanda hivyo," alisema.
Alisema eneo la hifadhi ya barabara ni moja ya maeneo hatarishi kwa yeyote atakayekimbilia kulitumia kwa kuwa hatakuwa na uhakika wa maisha yake na mali zake hasa kunapotokea gari kuacha njia.
Alisema mpango wa serikali kwenye maeneo hayo ya hifadhi ya barabara ni pamoja na kujenga vituo vya magari nje ya barabara kuu ili kuepusha magari makubwa kuegeshwa barabarani na kusababisha msongamano.
"Sisi kama wakala wa barabara tumepanga kujenga stendi nje ya barabara kuu kwenye maeneo yenye uhitaji ili kurahisisha magari kushusha abiria na kupakia bila bughudha kwa watumiaji wengine wa barabara," alisisitiza.
Masawe alisisitiza yeyote anayefanya biashara kwenye barabara ya akiba, anavunja sheria kwa kuwa watu wanatakiwa kukaa umbali wa mita 30 kutoka katikati ya barabara.
Mbali na ujenzi wa kituo cha mabasi, maeneo hayo ya hifadhi ya barabara yatatumiwa na TANROADS kuotesha miti na kutengeneza barabara za watembea kwa miguu.
Baadhi ya wananchi kwenye eneo hilo la Kisongo ambao waliathiriwa na bomoabomoa hiyo, waliipongeza TANROADS kwa kuboresha miundombinu yake, lakini wakaomba wasiharibiwe mali zao na kuomba waongezwe muda wa kufanya biashara ndogo bila kuweka vibanda.
"Kwa kweli hivi vibanda havistahili kuwapo kando ya barabara kuu na mimi ninaunga mkono zoezi hilo ila ninaomba hawa wafanyabiashara hususani kinamama wanaouza mboga na matunda waachwe waendelee kuuza bila kuweka vibanda," alisema Charles Lobulu, mkazi wa Kisongo.
Akiwa Kisongo, Meneja huyo wa TANROADS alikubali ombi hilo na kutoa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara hao wa mboga na matunda kuendelea kuuza bidhaa zao hadi mwishoni mwa mwezi huu.










