TAKUKURU yabaini kodi ya zuio milioni 83.3/- kutowasilishwa TRA

06Nov 2023
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
TAKUKURU yabaini kodi ya zuio milioni 83.3/- kutowasilishwa TRA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga, wamefanya uchambuzi wa mfumo wa Kodi ya zuio katika ununuzi wa vifaa na utoaji wa huduma zilizokatwa kutoka kwa wazabuni na kubaini kiasi cha Sh. milioni 83.3 hazikuwasilishwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo.

Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 06, 2023 na Kaimu Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Mwamba Masanja, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu.

Amesema kwa kipindi hicho wamefanya uchambuzi wa mfumo wa Kodi ya zuio katika mwaka wa fedha (2022/2023), na kubaini Sh.milioni 83.3 ikiwa ni fedha za Kodi ya zuio zilizokatwa kutoka kwa Wazabuni na watoa huduma hazikuwasiliswa TRA kama Sheria inavyoelekeza.

“Lengo kuu la uchambuzi huu ni kuona namna ya kudhibiti upotevu wa mapato husika, na kuanisha iwapo kuna mianya ya rushwa katika usimamizi wa ukataji wa kodi ya zuio asilimia mbili ya thamani ya bidhaa, na asilimia 5 kwa watoa huduma,” amesema Mwamba.

Ametaja sababu zilizosababisha kutowasilishwa fedha hizo za Kodi ya zuio TRA, ni kwamba imetokana na mabadiliko ya mfumo wa TRA (Tax Payer Portal), uelewa mdogo juu ya makato hayo, wazabuni na watoa huduma kutokudai stakabadhi za makato ya kodi ya zuio waliyokatwa, wahasibu husika hawakati kabisa kodi ya zuio kutoka kwa watoa huduma kinyume cha sheria ya kodi ya mapato.

Aidha, amesema wakati wa uchambuzi wa mfumo huo TAKUKURU ilizishauri Mamlaka husika kuwasilisha fedha hizo TRA kama Sheria inavyosema, na kwamba baadhi yao tayari wameshaanza kutekeleza, huku akibainisha kuwa wameshajipanga pia kukaa na TRA, wadau na watoa huduma kujadili matokeo hayo ya uchambuzi na kuweka mikakati ya pamoja kutatua changamoto hiyo.

Amesema kwa upande wa ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo, Taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji wa Miradi miwili, ambayo ni ujenzi wa Kituo cha Afya Bulige ambacho kipo Msalala wilayani Kahama, ujenzi wa shule mpya ya msingi Maganzo wilayani Kishapu, na kubaini mapangufu katika miradi hiyo, huku kituo cha Afya Bulige wakianza uchunguzi wa Awali,

Amesema katika ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Maganzo chini ya Mradi wa Boost wenye thamani ya Sh.milioni 561.1 wenyewe walibaini mapangufu katika jengo la Utawala kutowekwa Vigae, Mikanda ya Gypsum kubanduka, Roof ya board kuanza kutoa nyufa, na kwamba walitoa ushauri ili kurekebishwa mapangufu hayo.

Amesema kwa kipindi hicho pia wamefungua kesi tatu mpya Mahakamani, huku Kesi 5 za Uhujumu uchumi ziliamuliwa na washitakiwa wote walipatikana na hatia na kutolewa hukumu, na kwamba kesi 9 za zamani za makosa mbalimbali bado zenyewe zinaendelea Mahakamani.

Ametoa pia wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, kuendelea kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vya vitendo vya Rushwa ikiwamo Miradi ya Maendeleo, kwamba wafike katika Ofisi za TAKUKURU au kupiga simu bure 0738-150196 ili wazifanyie kazi na kuzuia vitendo hivyo kwa Maendeleo ya nchi.