Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya operesheni hiyo, Ofisa Ukaguzi wa TBS, Yona Afrika, alisema zaidi ya matairi 700 yameshakamatwa katika wilaya za Ilala na Temeke.
"Operesheni hii imekwishaondoa matairi zaidi ya 500 sokoni ingawaje katika wilaya ya Temeke tuliyaondoa machache baada ya wauzaji kuyaondoa wenyewe matairi hayo baada ya kusikia kuna operesheni hii," alisema Afrika.
Mmoja wa wauzaji wa matairi hayo katika wilaya ya Temeke, Ally Musa alisema biashara hiyo imekuwa ikimuingizia kipato na kumsaidia kuihidumia familia yake.
"Ninaitegemea biashara hii (na) nimeifanya kwa muda mrefu lakini operesheni hii inaturudisha nyuma kwani mzigo ukichukuliwa ni hasara kwangu, serikali isikie hili tunapata mahitaji mengi kwa kazi hii," alisema Musa.
Aidha TBS, imewataka wafanyabiashara hao kubadili aina ya biasha kwani operesheni hiyo itakuwa endelevu, ili kuziondoa bidhaa hafifu zisizo na ubora sokoni.
Ofisa Uhusiano TBS, Roida Andusamile, alisema awamu itakayofuata ya operesheni hiyo ni katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na kisha nchi nzima.
“Kiwango cha kimataifa cha matairi hakiruhusu matairi yaliyotumika sokoni, iwe ni kwa ajili ya matumizi ya baiskeli, magari, pikipiki," alisema na kutaka "Watanzania tubadilike kwani matairi yaliyotumika huwa chanzo cha ajali znazoongezeka nchini.”










