TADB yawashika mkono wahitimu waliofanya vizuri kimasomo SUA

22Nov 2023
Na Mwandishi Wetu
Morogoro
Nipashe
TADB yawashika mkono wahitimu waliofanya vizuri kimasomo SUA

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imewapongeza wahitimu bora wa Chuo Kikuu cha Kilimo Cha Sokoine (SUA) cha Morogoro kwa kuwapatia zawadi ya fedha taslimu shilingi milioni tano.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo ( wa pili kushoto) , Afisa Rasilimali Watu Mkuu wa Benki ya maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bi. Jacqueline Minja (wa tatu kushoto), wakikabidhi mfano wa hundi kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Kilimo Cha Sokoine (SUA) waliofanya vizuri zaidi ikiwa ni kama motisha kwao. Wanaoshuhudia kushoto ni Makamu Mkuu wa chuo SUA Prof Raphael Chibunda na kulia ni baadhi ya wafanyakazi wa TADB.

Motisha hiyo ya fedha, imetolewa na TADB kama sehemu ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri zaidi kupitia mpango mkakati wake mpya uliozinduliwa mwaka huu.

Akiongea wakati wa hafla ya kutoa zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri na wafanyakazi katika eneo la utafiti, Afisa Rasilimali Watu Mkuu wa TADB Jacqueline Minja alisema hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. 

“Benki yetu inatambua uwepo wa mikakati mbalimbali ya serikali kama vile sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 ambayo imetilia mkazo umuhimu wa kuweka mazingiza wezeshi kwa vijana kujihusisha na shughuli za kiuchumi, ikiwemo kilimo cha kisasa na kibiashara. Kwa kutambua hili, kwa kuanza, TADB imefika hapa na kutoa tuzo kwa wanafunzi bora mwaka huu.”

Afisa rasilimali huyo alieleza kuwa, katika awamu nyingine, benki itaandaa programu maalumu ya kuatamia vijana bora kutoka chuo kikuu cha SUA ilikutoa fursa ya kujifunza kazini. 

“Programu hiyo itakayokuwa ya miezi 24, italenga kutoa nafasi kwa wahitimu bora kuweza kupata nafasi ya kujifunza kazi kwa vitendo katika benki yetu,” alieleza Minja. 

Akizungumza katika mahafali hayo, Kaimu Mkuu wa Chuo Prof Raphael Chibunda aliishukuru TADB kwa kutoa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri pamoja na mpango wake wa kuandaa programu maalum ya kuwaatamia wahitimu wa fani ya kilimo.

TADB itaendelea kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) katika juhudi za kutengeneza vijana wabobezi katika sekta ya kilimo ili kuwezesha vijana kuchangia kufikia malengo ya serikali ya ‘Agenda 10/30’.