Maonyesho hayo yatakayojulikana kama ‘Mama Samia International Mkuranga Exhibition’, yamelenga mambo mbalimbali ikiwamo kuunga mkono juhudi za serikali ya Rais Samia katika kukuza uchumi wa nchi.
Taarifa iliyotolewa jana na Mratibu wa Taasisi hiyo, Omary Kombe, ilisema mbali na kuunga mkono juhudi za Rais, maonyesho hayo yatasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana na kuongeza pato la taifa.
“Maonyesho haya yana lengo la kutoa fursa kwa wawekezaji, wafanyabiashara wenye viwanda, sekta ya utalii na wajasiriamali wadogo kuuza biashara zao na kujitangaza kitaifa na kimataifa pamoja kuutangaza mkoa wa Pwani na taifa kwa kuwavutia wawekezaji na wafanyabiashara,” alisema Kombe.
Alisema kufanikisha maonyesho hayo yatakayokuwa na kaulimbiu ‘Tuko Tayari kwa Uwekezaji wa Viwanda, Biashara, Kilimo na Utalii Kazi Iendelee’, kiongozi huyo aliwaomba wadau wa maendeleo kujitokeza kudhamini maonyesho hayo ili kuunga mkono juhudi hizo.
“Naomba wadau wa maendeleo tujitokeze kudhamini maonyesho haya lakini ada kwa washiriki ni ndogo sana kulinganisha na maonyesho mengine. Mfano wawekezaji kutoka nje ya nchi watalipa Dola 500 za Kimarekani na wawekezaji wa ndani watatoa Sh. 500,000 kwa siku zote za maonyesho.
“Kwa wale wajasiriamali wa kati watalipia Sh. 100,000 na wale wadogo watalipia kuanzia Sh. 20,000 kwa hiyo fomu zitasambazwa kuanzia Septemba Mosi katika vyombo mbalimbali na maeneo maarufu hapa nchini,” alisema.
Maonyesho hayo tayari yameshapata kibali cha kufanyika kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Maendeleo ya Biashara.










