Akizungumza leo (Juni 4,2023) katika harambe ya kuchangia ujenzi wa shule mbili za Sekondari za Kiomboi na Kititimo iliyoandaliwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kati-Singida amesema ni lazima kuipeleka nguvu kazi kazini ili kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja kwani shughuli za uzalishaji ndizo zinazokuza kipato cha mtu mmoja mmoja.
"Ilikuwa inatokeaje kwamba nchi yetu ni tajiri lakini ina wananchi wake ambao ni maskini hii ni kwasababu shughuli ambazo zinaajiri watu wengi zinafanywa kizamani, kwamba watu wakivuna mara moja wakakosa chakula cha kutosha jawabu lake sio kuwapa chakula bali kuwafanya wavune mara tatu ndivyo walivyofanya nchi za Israel, Vietnam na nchi nyingine," amesema.
Dk. Mwigulu amesema katika kukabiliana na changamoto ya uzalishaji duni, Rais Samia Suluhu Hassan amepandisha bajeti ya kilimo mara nne ili kupeleka miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao jambo ambalo litawafanya wananchi kuvuna mazao kwa wingi na hivyo kuondokana na umaskini.
Amesema, kilimo ambacho hakitabiriki kilikuwa kinawafanya vijana waone kilimo si shughuli ya kufanya lakini mataifa yaliyoendelea tajiri anayesifika ni mtu ambaye yupo kwenye shughuli za sekta ya uzalishaji kama kilimo na ufugaji.










