Ulega alibainisha hayo juzi jijini Dodoma wakati wa kikao cha wizara na wadau wa tasnia ya kuku kilicholenga kujadili namna ya kukuza tasnia hiyo na utekelezaji wa sheria ya mwaka 2006.
Serikali imekuwa ikizuia uingizaji wa vifaranga kutoka nje ya nchi ili kudhibiti ugonjwa wa mafua ya ndege kwa mifugo jamii ya ndege na kulinda wazalishaji wa kuku ndani ya nchi.
Akifungua mkutano huo uliojikita katika upatikanaji wa vifaranga vya kuku, chakula cha kuku na bei ya kuku sokoni, Ulega alisema ni mategemeo kuwa serikali haitaona vifaranga vinaingizwa nchini kutoka nje ya nchi.
Ulega alisema wanataka kuwapo kwa mfumo wa taarifa zinazohusu wazalishaji wa vifaranga vya kuku kuanzia wazalishaji wakubwa hadi wadogo ambao wamesajiliwa na kutoa taarifa serikalini ili kuiwezesha kujua kiwango cha uzalishaji na takwimu sahihi kuhusu mahitaji ya vifaranga nchini.
“Ni mategemeo yetu baada ya Julai 30 mwaka huu kutokuona mtu anaingiza vifaranga nchini kutoka mahali popote pale.
"Jambo la pili kuwapo na mfumo ambao utasaidia serikali kujua ni kiasi gani cha uzalishaji vifaranga ndani ya nchi yetu ili kujipima uwezo wetu na mahitaji yetu ndani ya nchi,” alisema.
Awali Ulega alisema tasnia hiyo imekuwa kwa kasi miaka ya hivi karibuni kutokana na kuwaqpo kwa soko linalotokana na ongezeko la watu na kipato na ongezeko la uwekezaji na mazingira bora ya uwekezaji katika tasnia ya kuku.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Stephen Michael, alisema kutokana na umuhimu wa tasnia ya kuku katika Mpango Kabambe wa Sekta ya Mifugo wa Mwaka 2016, wamefanya tathmini na kubainisha kuwa hadi mwaka 2031, kutakuwa na upungufu wa nyama kwa tani milioni 1.8.
Kwa kuzingatia hali hiyo, alisema kuna haja kuchukua hatua, akisema tasnia hiyo ni rahisi na ikitiliwa mkazo, itasaidia katika kuongeza uzalishaji wa nyama nchini.
Michael ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Masoko katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, alisema ufugaji wa kuku ni njia rahisi na ambayo haihitaji maeneo makubwa na miundombinu mingi tofauti na mifugo mingine.
Alisema kikao hicho ni muhimu kwa kuwa kimeunganisha wadau wa tasnia hiyo pamoja na kutatua changamoto zilizopo kwa kuzingatia uwepo wa taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo kwa vijana na kinamama na vikundi mbalimbali ambao wengi wamejikita katika biashara ya kuku.
Katibu wa Chama cha Wadau wa Kuku Tanzania (PAT), Manase Mrindwa, alisema kero kubwa zinazowakabili ni chakula cha kuku kuwa kimefikia hadi Sh. 80,000 kwa mfuko mmoja na ongezeko hilo ni kutokana na bei ya mahindi na mashudu ya soya kwenye soko la Tanzania.
Kikao cha wadau wa tasnia ya kuku kilichoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kimejumuisha Menejimenti ya Wizara na Sekta ya Mifugo, wazalishaji wa vifaranga vya kuku, chakula cha kuku na wafugaji wa kuku ambao wametoa maoni mbalimbali ya namna ya kuboresha tasnia hiyo na kuomba kuwapo kwa vikao vya namna hiyo mara kwa mara ili kukuza tasnia hiyo kwa kuirasimisha na kuwapo kwa machinjio maalum kwa ajili ya kuku na bei elekezi ya kuku sokoni.










