Serikali yaridhishwa na ujenzi wa jengo la utawala

12Dec 2023
Shaban Njia
KAHAMA
Nipashe
Serikali yaridhishwa na ujenzi wa jengo la utawala

SERIKALI mkoani Shinyanga imeridhishwa na ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Ushetu linalogharimu kiasi cha Sh. Bilioni 5.320 ambalo hadi sasa limefika asilimia 84.

Jengo hilo linajengwa na Mkandarasi Mzinga Holding Co. ltd ya Morogoro kwa gharama ya Sh. bilioni 4.975, unasimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kama mkandarasi mshauri kwa mkataba wa Sh. Milioni 345.074

Aidha, hadi sasa jumla ya Sh. bilioni 2.856 ya gharama zimeshatolewa na ujenzi wake ulianza tarehe Mei 15, 2018 na unatarajia kukamilika tarehe Juni 05, 2024 ili lianze kuhudumia wananchi wa ushetu.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme ameyabainisha hayo leo wakati akikagua ujenzi wa jengo hilo lililojengwa kata ya Nyamilango nakusema ameridhishwa na ujenzi wake na litakuwa jengo la kisasa mkoa mzima lenye lifti katika majengo yaliyopo chini ya serikali za mitaa.

Aidha, amemtaka mkarasi kusimamia vyema vifaa vya ujenzi ili visiibiwe, ubora wa jengo na kuhakikisha wanapanda miti ya kimvuli na matunda kuzunguka jengo hilo ili wananchi wanapofika kupata huduma wapate mahala pa kupumzikia.

Akitoa taarifa ya ujenzi, Kaimu Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Alfred John amesema, ujenzi umefikia asilimia 84 na hatua zilizobaki ni ujenzi wa uzio, jengo la genereta, umeme, feni pamoja na kutengenza usawa kwa kundoa vifusi vilivyo kando ya jengo.