Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa anafunga mafunzo ya awali ya maaskari 700 wa Jeshi la Magereza ambao wamehitimu katika Chuo cha Magereza Kiwira wilayani Rungwe.
Alisema serikali imeshaanza michakato ya kurekebisha mashirika hayo ili kuendana na mfumo mpya wa uendeshaji kwa kushirikiana na taasisi zingine, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji na uendeshaji.
Alisema mageuzi hayo ya mifumo yanahusu uendeshaji pekee wa mashirika hayo na maeneo mengine ya majeshi hayo yatabaki kama yalivyokuwa awali.
“Tumeshaanza kuyafanyia mageuzi mashirika haya ili sasa yaendeshwe kwa mfumo wa ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi za kiraia (PPP), lengo la mageuzi haya ni kuongeza tija kwenye uzalishaji na mashirika yanayolengwa ni Shirika la Uzalishaji mali la Magereza na la Polisi,” alisema Masauni.
Alisema majeshi hayo yamechagua miradi mitano ya kuiendesha kwa utaratibu mpya utakaoanzishwa ili itumike kama dira kwa miradi mingine itakayoingizwa baadaye.
Masauni aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo kujiandaa kwenda kulisaidia taifa kupata maendeleo kwa kwenda kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia sheria za majeshi kama walivyofundishwa katika chuo hicho.
Mkuu wa Chuo cha Magereza Kiwira, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Rehema Mwailunga, alisema katika mafunzo hayo ya awali askari 700 walihitimu na walikuwa wameandaliwa vizuri kwa ajili ya kwenda kutumika na taifa.
Alisema kati ya wahitimu hao 580 ni wa kike na kwamba wahitimu hao wana ngazi mbalimbali za elimu kuanzia Kidato cha Nne mpaka Elimu ya Chuo Kikuu wakiwa wana ujuzi tofauti.
Alisema askari hao wamefundishwa mbinu mbalimbali za kijeshi na sheria ili wanapokwenda kwenye vituo vyao vya kazi wakafanye kazi kwa weledi na kulisaidia taifa.
“Wahitimu hawa kwa muda ambao tumekaa nao hapa wameonyesha uwezo mkubwa ambao unatupa picha kwamba watalisaidia taifa letu na kwa kuwa wamefundishwa miiko na maadili ya kazi tunaamini watafanya kazi vizuri,” alisema Kamanda Mwailunga.
Kamishna wa Magereza Nchini, Suleiman Mzee, alisema askari hao watasambazwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kwenda kutumika na kwamba hakuna askari hata mmoja kati yao ambaye atapangiwa kituo katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Aliwataka askari hao ambao asilimia kubwa ni vijana kwenda kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kufikia ndoto zao walizojiwekea.
Nao baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo waliahidi kwenda kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kulisaidia taifa kwa kutumia mbinu walizofundishwa katika chuo hicho.
Mmoja wa wahitimu hao, Mustapha Saddam alisema wamepata maarifa ambayo watahakikisha wanayatumia vizuri kwenye kazi zao pamoja na kuzingatia sheria na maadili ya kazi hiyo.










