Meneja wa TRA mkoani Lindi, Adamu Ntoga, aliliambia Nipashe ofisini kwake mjini hapa mwishoni mwa wiki kuwa meli hiyo yenye usajili namba 100066 na uzito wa tani 299, iliamatwa Februari mosi, mwaka huu ilipokuwa ikishusha bidhaa kutoka katika Bandari ya mjini Lindi.
Ntoga alizitaja bidhaa zilizokuwa zimebebwa na kushushwa kuwa ni mifuko 3,725 ya sukari kutoka nchini Brazil, mifuko 2,106 ya mchele, katoni 400 za biskuti, mafuta ya kula madumu 50 yenye ujazo wa lita 20 kila moja, katoni 59 za betri, hamira kavu katoni 20, baiskeri nane zilizotumika na majokofu manne ya mitumba.
Ntoga alisema baada ya kuzipitia nyaraka zinazoonyesha uhalali wa bidhaa hizo, walibaini kati ya madumu 80 ya mafuta ya kula, 50 yalilipiwa ushuru na 30 hayakulipiwa na mifuko 3,725 ya sukari inayodaiwa kuwa mali ya Makame, haikulipiwa ushuru wowote.
Aidha, alisema kati ya mifuko 3,087 ya mchele, ni 1,000 tu ndiyo iliyolipiwa na 2,087 haikulipiwa.
Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa bidhaa hizo, Masoud Ally na Salehe Yusufu, waliwatupia lawama mawakala wao wanaowaagiza kuwaletea mali hizo wakiwadai kuwa kwa upande wao hufuata sheria ikiwamo kuwapatia fedha za kulipia ushuru wa serikali.










