Mradi wa shamba la kuku kuongeza fursa za ajira

04Sep 2022
Anjela Mhando
Siha
Nipashe Jumapili
Mradi wa shamba la kuku kuongeza fursa za ajira

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki, amesema kuwepo kwa mradi wa shamba la wazazi wa kuku (Aviagen East Africa Limited) katika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro kutasiadia katika kuongeza fursa za ajira na maendeleo lakini pia kuongeza fedha za kigeni Nchini.

Waziri Ndaki ametoa kauli hiyo alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa shamba la wazazi wa kuku lililopo eneo la la West Kilimanjaro mradi ambao ni wakwanza kwenye ukanda wa Africa Mashariki na Kusini kwa Africa.

Kwa mujibu wa Waziri Ndaki amesema mradi huo utaongeza fedha za kigeni kwasababu wale wanaohitaji vifaranga wazazi wataagiza kutokana Nchini kwetu na sisi tutakuwa tunaingiza fedha za kigeni Nchini,ambapo amesema mradi huo unamanufaa makubwa kwa uchumi wa Nchi yetu.

Aidha, amesema zipo kazi za kitaalamu ambazo watoto wetu waliosoma ni nafasi ya mradi huu kutengeneza ajira ambapo amesema uwekezaji huo unaenda sambamba kauli ya Rais Samia Hassan kuwa anataka kutengeneza ajira million nane kufikia mwaka 2023 ndio maana nimesema tuukumbatie na tuulinde mradi huo kwani utatengeneza kipato kwa waajiriwa lakini pia utapanua sekta ya uzalishaji wa kuku .

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Thomas Apson, amesema Wilaya hiyo imepata bahati ya kupata uwekezaji huo ambao ni wakwanza Kuwepo Tanzania na umepatikana katika Wilaya hiyo ,ambapo amesema ni jambo kubwa kwasababu katika Afrika Mashariki na kati hakuna na kwa Tanzania nzima umepatikana Siha Kilimanjaro .