Mgomo wa daladala wasababishia Halmashauri hasara ya Sh.milioni 23

12Feb 2016
Nebart Msokwa
Nipashe
Mgomo wa daladala wasababishia Halmashauri hasara ya Sh.milioni 23

HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya imepoteza zaidi ya Sh. milioni 23 ndani ya miezi mitatu, kutokana na magari ya kusafirisha abiria ndani ya jiji hilo maarufu kama daladala, kugoma kulipa ushuru ili kuishinikiza serikali kuboresha barabara ambazo walikuwa wanadai kuwa ni mbovu.

OFISI ZA JIJI LA MBEYA

Daladala zilizosababisha hasara hiyo ni zile zinazofanya safari zake kati ya Uyole, Nsalaga, Igawilo, Ituha na Isyesye kuingia katikati ya jiji, ambazo ziligoma kulipa ushuru kutokana na ubovu wa barabara ya City Park ambayo ilikuwa imeharibika.

Mgomo huo umedumu kwa miezi mitatu kuanzia Novemba 2015 hadi Januari mwaka huu, baada ya dadadala hizo kugoma kuendelea kuitumia barabara ya City Park hali iliyoifanya Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa, Abbas Kandoro, kuamua kuzibadilishia ruti.

Akizungumza na Napashe, Ofisa Habari wa Jiji, John Kilua, alisema jiji lina vituo vinne vya daladala ambavyo vinakusanya ushuru huo.

Alivitaja vituo hivyo na idadi ya daladala zake kwenye mabano kuwa ni stendi kuu (300), Nanenane (50), Kabwe (120) na Sokomatola (42).

Kilua alisema jumla jiji hilo lina daladala 512 na kila moja inatakiwa kutoa ushuru wa Sh. 500 na kwamba kutokana na idadi hiyo jiji lilikuwa lilikuwa linapoteza Sh. 256,000 kwa siku ambayo ni sawa na Sh. 7,600,000 kwa mwezi.

Alisema baada ya madereva kugoma kulipa ushuru huo, jiji lilichukua baadhi ya adhabu lakini baada ya kuona kuwa madai yao ni ya msingi waliamua kuwaacha bila kukusanya ushuru huo ili kuweka mazingira ya majadiliano.

“Ilikuwa ni ngumu kwa sisi kufanya maamuzi ya kuendelea kuchukua hatua zaidi kutokana na kwamba sisi tunafanya kazi na watu kwa ushirikiano, hivyo tuliamua kuacha ili tuweke mazingira bora ya majadiliano na wadau wetu wa usafiri maana madai yao yalikuwa ni ya msingi,” alisema Kilua.

Hata hivyo, alisema barabara iliyowafanya madereva wa daladala hizo kugoma kulipa ushuru huo imeshatengewa bajeti na kwamba itaanza kutengenezwa baada ya mvua kupungua ili kurejesha tena daladala katika njia hiyo.