Mahakama yaelezwa wakili feki alivyonaswa

17Feb 2024
Grace Gurisha
Nipashe
Mahakama yaelezwa wakili feki alivyonaswa

OFISA wa Polisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO), Inspekta Sultan Mohamed, ameieleza mahakama kuwa mshtakiwa Baraka Mkama....

...alipohojiwa alitaja namba yake ya uwakili kuwa ni 4696 lakini ilipoingizwa kwenye mfumo likatokea jina la mtu mwingine ambaye anadaiwa kuwa ni Mwalimu wa Chuo Kikuu Dodoma.

 

Aidha, amedai kuwa wakili huyo feki alikamatwa katika viwanja vya mahakama hiyo Mei 23, 2023 baada ya kuzuia askari kutowakamata washtakiwa ambao kesi yao iliondolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya, kwa madai kuwa yeye ni wakili wao.

 

Ofisa huyo alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ushindi Swalo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakati akitoa ushahidi katika kesi dhidi ya Mkama anayedaiwa kujifanya ni wakili wakati akijua si kweli.

 

Alidai kuwa Mei 23, 2023 muda wa mchana, akiwa ofisi ya polisi ndani ya jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alisikia kelele za watu zikitokea geti la kuingilia mahakamani hapo.

 

"Nilienda getini na kumkuta askari Mbaraka akiwa ameshikana na mtu mwanamume aliyevalia suti nyeusi na skafu ya uwakili wa kujitegemea huku askari huyo akiwa amechubuka mkononi kwenye kiwiko," alidai.

 

Mohamed alidai kuwa kutokana na hali hiyo, alitumia busara kuwatuliza na kuwataka waende ofisini na kumuuliza askari kilichotokea na kumwambia kuwa mtu huyo alimzuia kukamata washtakiwa ambao kesi yao iliondolewa mbele ya Hakimu Mbuya.

 

"Wakati anataka kuwakamata mtu huyo aliyejitambilisha kama wakili wao, alimzuia kuwakamata ndani ya jengo na alimshambulia. Nilimhoji mtu huyo na akajitambulisha kuwa yeye ni wakili wa washtakiwa hao na ni mwanachama wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS),"alidai. 

 

Inspekta Mohamed alidai kwamba aliwapigia simu viongozi wake katika ofisi ya ZCO na walifika akiwamo Sajenti Stefano na gari na kumchukua mshtakiwa hadi kituo kikuu (central) kwa mahojiano zaidi.

 

"Akiwa bado yuko ofisi ya polisi katika Mahakama Kisutu, alifika mwakilishi kutoka TLS ambapo walikwenda wote ofisi ya ZCO alikopelekwa. Mshtakiwa alipohojiwa alitaja namba yake ya uwakili kuwa ni 4696. Baada ya hapo mwakilishi wa TLS aliingiza namba hiyo katika mfumo na likatoka jina la mtu mwingine ambaye anadaiwa kuwa ni mwalimu," alidai. 

 

Baada ya kueleza hayo, mshtakiwa alipopewa nafasi ya kumhoji shahidi huyo hakuwa na swali lolote dhidi yake.

 

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 11, 2024 kwa mashahidi wa upande wa mashtaka kuendelea kutoa ushahidi wao.