Katibu Mkuu Uchukuzi: Tumieni  Bandari ya Mtwara kwa shehena

07Nov 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Katibu Mkuu Uchukuzi: Tumieni  Bandari ya Mtwara kwa shehena

KATIBU Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, amesema uwezo wa Bandari ya Mtwara kwasasa kupokea shehena ya mizigo ni kubwa na ina mfumo wa kisasa, hivyo amewahamasisha mawakala kutumia fursa hiyo ipasavyo.

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Juma Kijavara akitoa maelezo ya kazi inayoendelea katika Bandari Kavu ya Kwala,Kulia ni Alexanda Ndibalema Afisa Mwandamizi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Akizungumza jana na wasafirishaji katika mpaka wa Tanzania na Zambia, amesema Bandari ya Mtwara inauwezo wa kushusha na kupakia makontena 25 kwa saa, hivyo ni fursa ya kupunguza msongamano Bandari ya Dar es Salaam.

Alisema kwa mawakala kutumia Bandari ya Mtwara ni faida kubwa kwao kwa kuwa itapunguza umbali wa safari kutoka Dar es Salaam na kuokoa muda wanaoutumia na hivyo kurahisisha biashara kwa pande zote.

Kwa mujibu wa Profesa Kahyarara, Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo kwa wadau wa korosho kuitumia Bandari ya Mtwara na kwa sasa inasafirisha makaa ya mawe yote yanayokwenda kwenye soko la dunia.

“Wasafirishaji wa mizigo kwenda Zambia na Malawi wataokoa muda mwingi unaotumika hivi sasa kusafiri kwa barabara umbali wa kilomita 800, kwani tayari serikali imeimarisha usafiri kuanzia bandari ya Mtwara mpaka Mbambabay kwenye Ziwa Nyasa,”amesema na kuongeza:

“Kutoka katika Bandari hiyo ya Ziwa Nyasa wanaweza kwenda mpaka Malawi Nkatabay au Lilongwe. Hiyo itapunguza umbali wa barabara muda wa safari na gharama. 

“Tayari kuna meli tatu katika Ziwa Nyasa Mbili za Mizigo MV Songea na MV Ruvuma ambazo zinauwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja na meli nyingine MV Mbeya ambayo inauwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za Mizigo.”

Katibu Mkuu huyo alisema mikoa ya Songwe Njombe, Iringa na Mbeya kupitia Ziwa Nyasa wanaweza kupitisha shehena zao Bandari ya Itungi au Kiwira. 

“Kama wanakutumia barabara wanaweza kutokea Ruvuma mpaka Njombe, serikali pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), tuko mbioni kukamilisha tathmini ya muda na gharama yaani ‘total Route Cost’ itakayotoa gharama na kiasi cha muda utakaonokolewa kwa watumiaji bandari ndani na nje,”amebainisha.

Aidha, Profesa Kahyarara amesema Rais Samia imedhamiria kuongeza mchango wa sekta ya usafirishaji  katika pato la Taifa, ajira na fedha za kigeni kwa namna nyingi ikiwamo kutumia fursa za kijografia kama uwepo wa Bandari ya Mtwara.

Serikali imewekeza vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhudumia meli za makasha, na Rais Samia alipotembelea bandari hiyo Septemba mwaka huu, aliagiza korosho zote kusafirishwa kupitia hapo.

Siku chache baadaye, Oktoba 22, mwaka huu, Bandari ya Mtwara ilipokea shehena ya kontena 300 iliyowasilia kwa ajili ya kusafirisha korosho ambazo hadi wakati huo tani 20,000 zilishauzwa kwa wanunuzi kutoka nchi mbalimbali.