Kanisa KKKT lawakumbuka wajane kwa kuwapa mtaji

16Jan 2024
Steven William
MUHEZA
Nipashe
Kanisa KKKT lawakumbuka wajane kwa kuwapa mtaji

KANISA la KKKT Usharika wa Muheza, limeamua kuwapa mtaji wajane ili waweze kufanya biashara mbalimbali za kustawisha uchumi wa familia zao.

Kadhalika kanisa hilo limeikumbusha jamii kuwajali wajane ikiwa ni njia mojawapo ya agizo la Mungu.

Wito huo ulitolewa jana na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Muheza mjini mkoani Tanga, John Ndimbo katika ibada ya Jumapili.

Ndimbo ameikumbusha jamii kukemea vitendo viovu ikiwamo udhalilishaji na ukatili wa kijinsia kwa wajane kwa kuwa hawakupenda kuwa katika hali hiyo.

Alisema kanisa hilo limeamua kuwakusanya wajane na kuwapa Shilingi milioni nne zitakazowasaidia kuanzisha mradi wa kukodisha maturubai na viti.

Alisema mwaka huu mpya wa 2024 kanisa lina ndoto kubwa ya kuanzisha miradi ikiwamo kujenga vibanda vya biashara kuzunguka kanisa na nyumba ya mchungaji eneo la Michungwani, Muheza.

Pia kanisa limeanzisha kitengo cha mwaka wa wanaume Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ambacho kitakuwa na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Katibu wa kitengo hicho cha mwaka wa wanaume Jackson Saria, alisema wamepanga kuanzisha mradi wa shule kuanzia darasa la awali pamoja na kununua vyombo vya muziki kwa ajili ya kwaya ya wanaume.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya fedha katika kanisa hilo, Bright Mshana, alitoa mchanganua wa mapato na matumizi mbalimbali ya bajeti katika kuendeleza miradi mbalimbali.