Sadiki na timu yake walifika katika eneo la mgogoro kwa lengo la kukutana na uongozi na wajumbe wa serikali ya kijiji cha Nanga, Mkuu wa Kituo cha Polisi Nanga na mtendaji aliyekuwapo wakati wa kubariki uuzwaji wa maeneo ya Jeshi la Polisi.
Mgogoro wa eneo hilo ulizuka kufuatia wananchi kuuziwa viwanja katika eneo la Jeshi la Polisi kwa madai kuwa uuzwaji huo ulikuwa na baraka za uongozi wa Kijiji cha Nanga na Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Igunga.
Akizungumza katika kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro huo, Diwani wa Nanga, Roberth Jidai, alisema kuwa yeye kama mwakilishi wa wananchi, alipelekewa hoja wananchi wameuziwa viwanja kwa kufuata taratibu zote, lakini wanazuiwa kufanya maendelezo kwa maelezo kuwa eneo hilo ni la jeshi, jambo lililomsukuma kutaka kulijua kwa undani.
Alisema kuwa baada ya kufuatilia kwa undani kwa kuiuliza serikali ya kijiji, alielezwa uuzwaji viwanja ni mradi wa serikali ya kijiji na ulibuniwa kwa lengo la kuupanga mji na kupunguza maeneo ya taasisi yaliyo makubwa na mpango huo ulishirikisha taasisi husika ikiwamo Jeshi la Polisi.
"Baada ya kuwa tumeapishwa, nililetewa hoja hii na wananchi zaidi ya 30 wakiwa na hati za viwanja na nilitaka kujua ilikuwaje na baada ya kuuliza nilielezwa na serikali ya kijiji kuwa huo ulikuwa mradi wa serikali ya kijiji wenye lengo la kupunguza maeneo ya taasisi ambayo ni makubwa," alisema.
Kufuatia maelezo ya uongozi wa kijiji na kukagua baadhi ya nyaraka za mauziano ya viwanja, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tabora, Sadiki, alibaini kijiji kilikaa kikao kwa madhumuni ya kumega maeneo ya umma. Eneo la Jeshi la Polisi lilimegwa na kutolewa vipande 51 vya ardhi.
Hata hivyo, upimaji wa vipande hivyo haukupata idhini na hakukuwa na mpango mji ulioidhinishwa. Baadhi ya wajumbe walikuwa wanufaika wa mpango huo.
Kamishna Sadiki aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa kikao kilichofanya uamuzi kuchukua na kuuza viwanja eneo la polisi hakikuwa na mamlaka hayo na kilichofanyika ni batili.
"Kikao chao kile hakikuwa na mamlaka ya kumega maeneo ya taasisi. Maeneo yanayomilikiwa na serikali yaheshimiwe, iwe kwa taasisi yoyote na hakuna kikao cha kijiji chenye mamlaka ya kusema tunamega eneo la taasisi," alisema Sadiki.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nanga, Henry Masanja alisema kuwa kufuatia kadhia hiyo, aliomba mamlaka zenye jukumu la kusimamia mamlaka zilizo chini kuhakikisha zinatoa ushauri mzuri kwa mamlaka za chini kwa kuwa kilichotokea ni ushauri mbaya kutoka mamlaka ya juu.
Mjumbe wa Serikali ya Kijiji, Lawrence Kishiwa alieleza kuwa tatizo ni wajumbe wanaochaguliwa kutopewa elimu kuhusu miiko na mipaka yao ya utendaji kazi.
Aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nanga, Ambele Mwangomo ambaye alialikwa katika kikao hicho kutokana na kuwa kiongozi wakati wa uuzwaji viwanja, alieleza mbele ya kikao hicho kuwa, amejifunza viongozi wa serikali wanaoshirikiana na wananchi katika kutoa huduma kwa jamii wanapaswa kufuata misingi vizuri na sheria inavyoelekeza.
"Kwa ngazi yetu kama serikali ya kijiji tulitekeleza hilo kutokana na kutoelewa vizuri taratibu zinakwenda vipi, tukaendelea kuwasiliana na mamlaka ya wlaya, yaani wataalamu wa ardhi na kulisimamia hilo tukidhani tuko sahihi," alijutia.
Akihitimisha kikao hicho, Kamishna Sadiki alisema ni lazima viongozi wajionye katika nafsi zao hasa pale wanaposhughulika na mali za serikali.
"Ni hatari iwapo viongozi mliopewa dhamana mnabariki kumega na kujigawia maeneo ya umma. Ni batili. Kazi tunayokwenda kuifanya ni kupitia kila mmoja anayesemekana alipatiwa eneo hili. "Hatutaruhusu yeyote kunufaika na ubatili uliofanyika hali ya kuwa ameshiriki katika kikao kilichoazimia kukata maeneo ya umma. Eneo la polisi litabaki kuwa la polisi," alisema.










