Balozi Vehineh alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa maadhimisho ya miaka 45 ya Mapinduzi ya Iran, ya mwaka 1979, yaliyouondoa utawala wa kifalme na kusimika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika katika makazi ya Balozi, jijini Dar es Salaam, Balozi Vehineh amesema kuwa mwaka uliopita kiwango cha biashara kati ya nchi hizo kilikuwa Dola za Marekani 60 milioni sawa na Sh. bilioni 150.3.
Amefafanua kuwa, Iran iliingiza nchini bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 40 sawa na Sh. bilioni 100.2, huku ikiagiza bidhaa kutoka Tanzania zenye thamani ya Dola milioni 20 sawa na Sh. bilioni 50.1.
Ameeleza kuwa, kutokana na hatua zinazochukuliwa za kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande zote, wanatarajia kuwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kitaongezeka katika siku chache zijazo.
Amesema kuwa bado kuna maeneo muhimu ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili yakiwamo ya kilimo, migodi, uvuvi, ufugaji na sayansi na teknolojia.
Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Omar Said Shaaban, ametoa wito kwa pande zote kuongeza juhudi kuimarisha ushirikiano katika eneo hilo la biashara na uwekezaji.
Amebainisha kuwa Tanzania chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ilikuwa ni Taifa la kwanza la Kiafrika kuipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Mapinduzi ya mwaka 1979, kuanzia hapo uhusiano na ushirikiano huo umeendelea kukua siku hadi siku katika sekta mbalimbali.
Hata hivyo, amesema kuwa kiwango cha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji, kwa hivi karibuni kimepungua.
“Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Viwango (TBS), kiwango cha uwekezaji na biashara kati ya nchi hizo mbili kimepungua kutoka Dola 18.8 milioni sawa na Sh. bilioni 47 mwaka 2017 mpaka Dola milioni 2.8 sawa Sh. bilioni 7 bilioni mwaka 2022,” amesema Shaaban.









