Amesema kwa sasa wakulima wanakopa kwenye benki ambazo zina mrengo wa kibiashara, hivyo kuna haja ya kuwa na sera ya fedha itakayohusu sekta hiyo itakayotoa fursa ya wakulima kuwa na uwezo wa kukopesheka kwa urahisi bila kuwapo vikwazo vinavyosababishwa na kutokuwapo sera maalum ya fedha kwenye kilimo.
Ameyasema hayo mkoani Tabora baada ya kuzindua tawi jipya la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambalo litahudumia mikoa mitatu ya Tabora, Kigoma na Katavi.
Alisema kuwapo benki hiyo kutasaidia kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo katika ukanda huo wa magharibi.
"Katika uchumi wote wa nchi yetu, mikopo inayoingia ni zaidi ya Sh. trilioni 20 na inayokwenda sekta hii ni asilimia chini ya 10. Na bado ukienda kwenye uzalishaji katika kilimo fedha inayotolewa kama mkopo ni ndogo sana.
"Sasa nimeshaongea na Waziri wa Fedha, Gavana wa Benki Kuu, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, ninawaandikia barua.
"Tunahitaji sera ya fedha ya kilimo kwani haiwezekani kilimo kikopeshwe kwa kutumia sera za benki za biashara, kutumia sera hiyo bado hatutoweza kutoa watu kwenye umaskini," amesema Bashe.
Ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada za kuinua sekta hiyo na kuboresha maisha ya wakulima, ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji na kupanua huduma za benki ya kilimo yenye lengo la kuleta mapinduzi ya kilimo kwa mipango endelevu inayokidhi mahitaji ya wakulima kupitia huduma tofauti za kifedha.
"Serikali ikishamaliza kuboresha miundombinu mkulima anahitaji fedha ya kununua mbolea na pembejeo. Kwa hiyo, ni muhimu na lazima tukawa na sera inayoeleweka ya kupata mitaji kwenye sekta za uzalishaji kama kilimo, mifugo na uvuvi, na mimi kama waziri nitawasukuma wote wanaohusika ili kupata sera hii na ninaamini itafanikiwa," amesisitiza Bashe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TADB, Frank Nyabundege, amesema hadi kufikia Februari, mwaka huu, TADB imewezesha wakulima na wafugaji kwa kutoa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 19.599 katika mikoa ya Kigoma Sh. bilioni 7.209, Katavi Sh. bilioni 2.394 na Tabora Sh. bilioni 9.996.
"Mikopo hii imetolewa kwenye miradi ya mpunga, michikichi, maharage, mahindi, unenepeshaji ng’ombe, tangawizi, ufugaji kuku, nguruwe na kondoo.
"Benki inaendelea kuweka mikakati thabiti ya kukopesha kwenye zao la tumbaku, pamba na asali, kwani mazao haya yanachangia kukuza uchumi wa Mkoa wa Tabora," amesema Nyabundege.
Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Vyama vya Ushirika Kigoma, Hussein Buchunguka, ambaye ni mkulima wa mchikichi, ameshukuru benki hiyo kwa mchango mkubwa wa kuwawezesha wakulima na katika ununuzi wa mitambo ya uchakataji wa zao hilo.
"Leo mchikichi unatambulika, awali lilikuwa zao la mazoea, sasa ni zao la uchumi mpaka tunavyoongea mtayaona mafuta yanayotokana na mchikichi, safari ya kuondokana na uhaba wa mafuta imeanza, asanteni kwa kutuunga mkono na kujenga heshima yetu katika kilimo," amesema Buchunguka.










