Kutokana na kuonyesha kiwango kizuri na kuipa timu yao taji la tatu la michuano hiyo, vijana hao waliamini na kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza. Miongoni mwao ni straika anayeibeba Simba kwa sasa Ibrahim Ajibu.
Mshambuliaji huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji wawili waliopiga 'hat-trick' Kombe la Mapinduzi akiunga na Mfungaji Bora, Simon Msuva (mabao manne).
Ajibu ameenza 'kuienzi' michuano hiyo baada ya juzi kufunga bao pekee lililopa Simba ushindi wa 1-0 dhidi ya URA ya Uganda kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.
Akiwa hatua mbili kutoka kwenye boksi la lango la kusini, Ajibu alitupia kwa kupiga shuti kali la mguu wa kulia baada ya kupewa pasi murua na kiungo Mwinyi Kazimoto katika dakika ya 37 ya mchezo, likiwa ni bao la 20 la michuano hiyo mwaka huu.
Ajibu amekuwa mchezaji wa tatu kufunga goli la shuti la nje ya boksi kwenye michuano nje ya boksi akitanguliwa na Osca Agaba wa URA (dhidi ya JKU) na Kipre Tchetche wa Azam FC (dhidi ya Yanga).










