Abiria 1,000 wa treni wakwama Dodoma mafuriko yakisomba reli

04Jan 2016
Nipashe
Abiria 1,000 wa treni wakwama Dodoma mafuriko yakisomba reli

Zaidi ya abiria 1,000 wa treni ya abiria waliokuwa wakielekea Dar es Salaam, jana walikwama kuendelea na safari yao kutokana na reli kusombwa na mafuriko katika stesheni ya Kidete na Mzaganza.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa

Abiria hao walikwama mjini Dodoma wakitokea Mikoa ya Kigoma, Mwanza na Tabora wakielekea Dar es Salaam na Morogoro.

Kufuatia hali hiyo, uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), ulilazimika kukodi mabasi 17 kwa ajili ya kuwasafirisha abiria hao kwenda Dar es Salaam.

Mkuu wa usafirishaji abiria na mizigo Dodoma, Haruna Mwano, alithibitisha kukwama kwa abiria hao huku akisema uongozi wa TRL umeshafanya utaratibu ili abiria hao waendelee na safari.

"Ni kweli abiria takriban 1,090 wameshindwa kusafiri ni wa kutoka Mikoa ya Kigoma, Mwanza na Tabora kuelekea Morogoro na Dar es Salaam na wamekwama katika stesheni ya Dodoma kutokana na reli kusombwa na mafuriko," alisema Mwano.

Alifafanua kuwa abiria hao walianza safari juzi jioni na wamerudishiwa fedha ya chakula ili wajikimu wawapo njiani kuelekea Dar es Salaam.

Alisema wametumia mabasi 17 kusafirisha abiria hao na bado hajajua huduma zitarejea lini katika hali yake ya kawaida.

Wakati huo huo, uongozi wa TRL, umetangaza kusitisha kwa muda kuanzia Januari mosi, mwaka huu kutoa huduma zake za usafiri baada ya eneo la reli kati ya Kilosa mkoani Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma kutokana na tuta la reli kukumbwa na mafuriko.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Mhandisi Elias Mshana, taarifa za kiufundi eneo lililoathiriwa na mafuriko ni kubwa, hivyo wahandisi na mafundi wa TRL wako eneo la mafuriko kutathmini ukubwa wa kazi yenyewe.

Aidha, ilisema uongozi utatoa taarifa kamili kuhusu lini huduma za TRL kwenda bara zitaanza tena.