Kwa haya Jeshi la Polisi lijitathmini

27Aug 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kwa haya Jeshi la Polisi lijitathmini

JUZI Rais Samia Suluhu Hassan, aliweka bayana kilio cha wananchi dhidi ya utendaji kazi wa askari polisi kwa kubambikia kesi raia, kuwekwa mahabusu kwa muda mrefu, kutokutenda haki na kuwatesa wanapokuwa mikononi mwao.

Rais aliyataja baadhi ya mambo ambayo ni lazima Jeshi la Polisi liyaangalie kwa jicho jingine na ambayo amekuwa akiyarudia kwa zaidi ya mara tatu kuwa ni kubambikia watu kesi na kuwaacha wateseke kwa muda mrefu bila sababu.

Aidha, alisema ucheleweshaji wa upelelezi unaongeza mzigo mkubwa kwa serikali kuweka mahabusi jela na kwamba kwa mujibu wa takwimu za Agosti 22, mwaka huu, kwenye jela kulikuwa na wafungwa 16,542 huku mahabusi wakiwa 15,194.

Alilitaka jeshi hilo kuangalia kesi ambazo wanaona upelelezi wake hautokamilika, watuhumiwa watolewe jela wakafaidi uhuru wao wakiwa nje, huku akitaka upelelezi kukamilishwa ndani ya miezi sita hadi mwaka.

Alitolea mfano wa nchi nyingine duniani kwamba mtu hakamatwi mpaka upelelezi umetimia, akikamatwa anawekwa ndani wiki, siku tatu, nne anapelekwa mahakamani, lakini kwa Tanzania hali ni tofauti kwa kuwa wapo wanaokaa kwa muda mrefu.

Tunamshukuru Rais kwa kutambua haya ambayo kimsingi ni kilio cha muda mrefu cha wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi nchini, licha ya kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda raia na mali zao, lakini inaingia doa kutokana na matendo ambayo huumiza wananchi.

Wapo watu wanaosota rumande kwa zaidi ya wiki mbili kwa kunyimwa dhamana, huku wengine wakisota rumande kwa miaka na miaka, sababu kubwa ni kutokamilika kwa upepelezi. Hata hivyo, baadhi ya kesi zinaendeshwa kwa haraka, jambo ambalo linaonyesha iwapo kutakuwa na uwajibikaji, kesi zinaweza kukamilishwa kwa wakati.

Kimsingi, uwapo wa maabusu wengi una athari kwa mhusika na familia yake pekee, bali pia kwa taifa kwa kuwa ni gharama kubwa kuwatunza kuanzia chakula na huduma nyingine za kijamii, huku kukiwa na askari wanaolipwa mishahara na stahiki nyingine, mafuta ya magari, vipuri na ankara za maji na umeme.

Gharama hizi zingeweza kupunguzwa ikiwa upelelezi utafanyika kwa wakati na itasaidia serikali kuondokana na mzigo wa kuhudumia watu ambao wangeweza kuzalisha mali au kuendelea kuwa uraia wakizalisha kwa faida yao na taifa.

Lakini kuendelea kubambikia kesi, kunyanyasa na kuwaumiza watu na kuwasababisha vifo kwa namna yoyote ile kunaendeleza chuki na visasi visivyo vya lazima, kwa kuwa bado kuna uwezekano wa kujifunza kwa nchi zilizoendelea zinavyokabiliana na mambo haya na kuiga kwa yale yanayofaa.

Yapo matukio ya ndugu kulalamika na mengine kuthibitishwa kuwa wamepoteza maisha wakiwa mikononi mwa polisi kutokana na kipigo kikali, huku baadhi ya askari wakiwajibishwa juu ya hayo, lakini yameendelea, hivyo kuchafua taswira ya jeshi hilo.

Rais amerudia mara kadhaa na sasa ameshauri kufanya mabadiliko ya sheria kuhakikisha haki inakuwapo kwa kuwa kila anayetuhumiwa ana haki hadi pale Mahakama itakapothibitisha makosa yake, na hata akihukumiwa kuna haki zake pia.

Ni muhimu Polisi wakajisafisha dhidi ya malalamiko ya muda mrefu kuwa badala ya kuwa msaada sasa wamegeuka kuwa maumivu, kiasi cha watu kuona hakuna sababu ya kwenda polisi pale jambo linatokea kutokana na imani zilizojengwa au kujengeka miongoni mwa wananchi.

Tupo kwenye dunia ya utandawazi ambayo watu wanapata mambo mengi kwenye mitandao ya kijamii, ni muhimu sana Jeshi la polisi likajisafisha kwa kuondoa wanaolichafua kwa kurejesha imani kwa wananchi kuwa wao ni kimbilio na siyo sehemu ya maumivu kwa wale waliokwisha umizwa.

Mkuu wa nchi ameona mengi ameyasema hadharani, sasa ni wakati wa jeshi hilo kujitathmini juu ya yote ambayo yanalalamikiwa, kusafisha wale wasio waadilifu ambao wamegeuza vituo vya polisi kama sehemu ya maumivu au kupiga dili dhidi ya raia wema.