Malalamiko yalitolewa na wazazi mtandaoni, kutuma ujumbe mfupi wa maandishi huku mwanafunzi mmoja akivaa mabango yenye ujumbe na kukaa juani kufikisha ujumbe wa kutoridhika na tahasusi pamoja na shule aliyopangiwa kuendelea na kidato cha tano.
Kutokana na malalamiko hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, alitumia mitandao yake ya kijamii kujibu kwa mifano hoja mbalimbali za wazazi, na kusisitiza kuwa walichopangiwa wanafunzi ndicho walichochagua katika chaguo la kwanza hadi la tano.
Wapo wazazi waliolalamika kuwa watoto wao walichagua kuendelea na kidato cha tano, licha ya kuwa na ufaulu wa daraja la kwanza, lakini bado walipangiwa kujiunga na vyuo vya diploma.
Pia, wapo waliolalamika kupangiwa shule na tahasusi ambazo hawakuchagua na kwenye mitandao ya kijamii alijaribu kumwonyesha waziri kuwa kilichofanyika sicho.
Kimsingi licha ya ufafanuzi wa serikali bado inaonyesha kuna tatizo mahali hasa katika kuchagua na kupanga wanafunzi, kwa kuwa bado inafikirisha aliyepata daraja la kwanza imekuwaje anapangiwa kwenda chuo wakati hakupenda kwenda huko.
Lakini mara nyingi imekuwa ndiyo utaratibu kwamba wenye ufaulu mdogo wanakwenda kusoma sayansi, huku wenye ufaulu mkubwa wakienda kusoma ualimu.
Pia, kuna dhana kuwa ambaye hakuendelea na kidato cha tano maana yake hakufanya vizuri kwenye mitihani yake, na hili ni muhimu sana likatolewa ufafanuzi kwa kuwa limesababisha matabaka kwenye elimu hadi ajira.
Inaaminika kuwa mwanafunzi aliyesoma hadi kidato cha sita ni bora zaidi ya aliyesoma diploma kisha akaenda chuo kikuu, na hii inadhihirisha kuwa ni lazima mfumo wa elimu utazamwe upya, kwa kuhakikisha unapika wataalam bora kwa taifa.
Kama ambaye hajafanya vizuri ndiye anapangiwa kusoma ualimu maana yake tumefundishwa, wanafundishwa na watafundishwa na watu ambao hawajakidhi matakwa sahihi, na kama ndiyo utaratibu maana yake aliyefeli ndiye anapaswa kuandaa mtaalam ambaye atakwenda kufundisha waliofanya vizuri.
Lakini ni muhimu huu utaratibu wa kuchagua cha kusomea ukatoa nafasi kwa wanafunzi wenyewe baada ya kuelimishwa vyema kutambua ni nini anakwenda kusomea, atafanyakazi gani na asipangiwe kingine ambacho hatakiweza.
Madhara ya kupangiwa kwa sababu ya utaratibu au wazazi kutaka mtoto wao awe kama fulani ni makubwa kwa kuwa kuna hatari kubwa ya kuwa na wataalam ambao wamesomea walichosomea kama njia ya kupita na siyo kwamba wanapenda kazi husika.
Mathalani, kuna wakati kulikuwa na wimbi la wanafunzi kujiunga na ualimu kwa kuwa ilikuwa njia ya kupita ili kupata ajira kwa haraka na baada ya hapo anaomba ruhusa kwenda masomoni kusomea kitu kingine na baadaye harudi kituo cha kazi, lakini kwa muda wote anaendelea kulipwa mshahara.
Ni muhimu sana serikali ikaangalia suala la upangaji wa tahasusi ili kuhakikisha mwanafunzi anasomea kile anachokipenda, na kuwe na ufafanuzi mzuri wa nani anayetahili kusoma diploma na anayestahili kuendelea na kidato cha tano, ili kuondoa matabaka ya kwamba kuna aliyebora na wasiobora ambao wote watakutana vyuo vikuu.
Je inapofika kwenye ajira kinachoangaliwa ni njia uliyopita kupata utaalam fulani au ni kiwango cha ufaulu wako na sifa inayokufanya ubaki kazini? Yote haya yafafanuliwe ili wanafunzi akipangiwa vyuo wazazi na wanafunzi wasione shida.










