PPP imekuwapo miaka mingi na kuna miradi ambayo ilitekelezwa kwa muundo huo, lakini haikuwa na mafanikio makubwa kutokana na kukosekana mazingira wezeshi yenye kuelekeza taratibu za kufuata katika kufanya maandalizi kabla ya kuingia mikataba.
Kutokana na hali hiyo, serikali iliandaa sera na sheria ya PPP ili kuwa na utaratibu wa kushirikisha sekta binafsi kwa kutumia dhana hiyo.
Katika kufanikisha mabadiliko ya sasa kwa lengo la kutekeleza mpango huo kwa tija na ufanisi, kilichofanyika ni kuwa na timu ya watalaamu zilizoundwa kutoka taasisi mbalimbali za serikali kufanya uchambuzi wa miradi 41 kati yake imeandaliwa na kufanyiwa uchambuzi na Mamlaka za Serikali kutoka sekta mbalimbali na mradi mmoja umeandaliwa na mwekezaji kutoka sekta binafsi.
Hizi ni habari njema kwa Watanzania kwa tunaamini PPP ina mambo mengi mazuri kama kuongeza ajira, mapato, uzoefu, ubunifu na teknolojia, kwa kuwa hakuna ubishi kuwa asilimia kubwa ya ajira zinatokana na sekta binafsi.
Ni ukweli pia serikali zote duniani haziwezi kufanya biashara bali jukumu ni kuweka mazingira mbalimbali wezeshi.
Tunatarajia kuwa programu hiyo itakuja na mambo mazuri, ambayo yataonyesha tofauti ya zamani na sasa, kufukia mashimo yote yaliyojitokeza awali ikiwamo kuisababishia serikali hasara ilipokuwa inabinafsisha au kukodisha mashirika ya umma. Tinaamini pia kwamba hatua hii unatoa nafasi kwa Watanzania kunufaika.
Tunaamini sekta binafsi ikishirikishwa vyema tutaona ukuaji wake, ikiwamo kutoa mchango wake kwa maendeleo kwa taifa, ikiwamo kuongeza mzunguko wa fedha.
Pia, itasaida ukuaji wa teknolojia kwa manufaa ya taifa, ikiwamo kujifunza mambo mapya yanayotokea duniani, kwa maendeleo endelevu.
Tunatarajia kutakuwa na uwazi na ushirikishwaji ipasavyo kwa Watanzania ili kuomba kushiriki kwenye utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo itakuwa na matokeo chanja kwa taifa.
Katika hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi Wizara ya mwaka 2021/22 imeweka vipaumbeele 13 huku kimojawapo kikiwa ni kuimarisha na kuboresha mfumo wa PPP kwa manufaa ya taifa.
Tuna hakika iwapo kutakuwa na usimamizi thabiti, ufuatiliaji, uwazi na uajibikaji kwa pande zote maana yake miradi yote itakayotekelezwa itakuwa na tija.
Nchi nyingi duniani zimepiga hatua kutokana na kuishirikisha sekta binafsi kikamilifu, na sasa ni wakati wa kuhakikisha inasonga mbele na kushika kasi ili kuona tofauti ya miradi inayotekelezwa na sekta binafsi na mingine.










