Mbeya Kwanza, Geita Gold maandalizi Ligi Kuu ni sasa

07Jun 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mbeya Kwanza, Geita Gold maandalizi Ligi Kuu ni sasa

MBIO za kuwania kupanda Ligi Kuu Bara hatua ya makundi kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza, tayari zimehitimishwa kwa Mbeya Kwanza FC na Geita Gold FC kukata tiketi ya moja kwa moja baada ya kuibuka vinara katika wa Kundi A na B.

Timu hizo zimepanda moja kwa moja na zilizoshika nafasi ya pili Pamba FC na Transit Camp zikisubiri kujua wapinzani wao kutoka Ligi Kuu watakaokutana kwenye mechi ya mchujo kuwania nafasi mbili zilizosalia ili kukamilisha timu 16 zitakazoshiriki ligi hiyo msimu ujao.

Tayari Shirikisho la Soka nchini (TFF), limechezesha droo ya mechi hizo za mchujo, ambapo Pamba FC ya Mwanza itamenyana na timu itakayomaliza nafasi ya 13 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu huku Transit Camp ikimenyana na timu itakayomaliza nafasi ya 14 katika ligi hiyo.

Hivyo, huu ni wakati kwa Pamba na Transit Camp kuendelea kujifua kwa nguvu zikisubiri kujua wapinzani wao hao kuelekea mechi hizo, zitakazochezwa Julai 21, mwaka huu kabla ya kurudiana siku tatu baadaye.

Kwa upande wa Mbeya Kwanza na Geita Gold ambazo tayari zina tiketi ya kushiriki Ligi Kuu msimu ujao, zinapaswa kutambua haitakuwa ligi nyepesi, hasa kutokana na timu kupunguzwa kutoka 18 hadi 16, lakini pia ikiongezewa thamani baada ya Kampuni ya Azam Media kuongeza dau la udhamini wa kurusha matangazo.

Kwa ujumla, Nipashe tunatambua itakuwa ligi ngumu sana na yenye ushindani mkubwa kuanzia mwanzo hadi mwishoni mwa msimu, hivyo kama timu zilizopanda na zitakazopanda hazitajipanga mapema, kuna uwezekano wa kuwa za kwanza kurejea zilipotoka.

Katika kipindi hiki ligi ikiendelea, ni wakati wa makocha wa timu hizo kuifuatilia kwa makini na kutazama wachezaji wakuweza kuboresha vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao, badala ya kusubiri wale ambao watatemwa kutokana na viwango vyao kushuka.

Tunatoa tahadhari hiyo mapema kwa kuwa imekuwa kawaida kwa timu zinazopanda Ligi Kuu, kuvizia wachezaji wanaotemwa kutokana na kushuka viwango, ili kuimarisha vikosi vyao, jambo ambalo zinazifanya kushindwa kutoa ushindani mkubwa katika mbio za ubingwa, hivyo kubaki kwa 'farasa' watatu; Simba, Yanga na Azam, ambazo zimekuwa zikipokezana taji hilo kwa kipindi kirefu.

Nipashe tunatamani kuona timu zinazopanda Ligi Kuu zikija kutawala na kutoa changamoto kwa zilizopo ili ligi izidi kuwa ya kiushindani, hivyo ili hilo litimie, ni wakati kwao wa kuingia katika soko la usajili kwa kuchomoa wachezaji wenye uwezo mkubwa na si kusubiri wanaotemwa kutokana na kushuka viwango.

Lengo letu ni kuona Ligi Kuu Tanzania Bara ikitoka katika nafasi ya nane kwa ubora barani Afrika na kupanda juu zaidi, na hilo linawezekana tu kwa kila klabu kujipanga vema katika uwekezaji hususan kwa kusajili wachezaji wenye viwango vya hali ya juu ili kwenda kutoa ushindani wa kweli.

Aidha, hatutaki kuona timu zilizopanda zikiwa za kwanza kupigania kujinasua katika msitari wa kushuka daraja mwishoni mwa msimu kama ilivyo sasa kwa Gwambina FC inayoshika nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu, hii ikiwa ni mara yao ya kwanza kushiriki ligi hiyo.

Katika hili, hakuna muujiza zaidi ya kila timu kujipanga ipasavyo kuelekea ligi hiyo, huku zikitambua kutegemea wachezaji waliozipandisha daraja pekee bila kuwaongezea wazoefu, kutaziweka katika wakati mgumu wa kuweza kutoa ushindani ligi hiyo itakapoanza msimu ujao.

Mfano halisi ni Ihefu FC, ambayo kama si kufanya maboresho kwa kusajili wazoefu katika usajili wa dirisha dogo, ilikuwa ikichungulia 'kaburi' la kushuka daraja, kabla kujinasua mzunguko wa pili ingawa bado nafasi ya 12 iliyopo kwa sasa haijawa salama sana kutokana na kutofautiana pointi moja tu na timu nne zinazoifuata.