Tasaf ilianza kutekeleza mpango wa kuzinusuru kaya maskini katika awamu ya tatu mwaka 2012, lengo likiwa ni kupunguza ukali wa maisha kwa kuziwezesha kaya maskini sana ambazo zimeingia kwenye mpango kuibua miradi, kuongeza kipato, uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu na kujenga rasilimali watu miongoni mwa watoto kwa kutimiza masharti ya Elimu, Afya na Lishe.
Walengwa wa mpango wa Tasaf awamu ya tatu ni kaya zote zenye watu ambao ni maskini na wasiyojiweza, kaya maskini sana hususani zenye wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, watoto wanaosoma shule za awali, msingi na sekondari.
Wengine ni kaya ambazo ziko kwenye maeneo yaliyoathirika na majanga mbalimbali kama vile ukame, mafuriko au gharama kubwa ya chakula.
Pamoja na lengo zuri la Serikali la kuzinusuru kaya maskini kwa kuzipatia fedha kwa ajili ya kupata mahitaji muhimu ya afya, elimu, lisha pamoja na kuanzisha shughuli za kujipatia kipato, jambo la kusikitisha ni kwamba baadhi ya walengwa wa mpango huo wanakiuka masharti ya matumizi ya fedha hizo na kujikuta wakipoteza sifa za kuwa walengwa.
Kwa mfano, zimeripotiwa taarifa nyingi karibu maeneo yote ya nchi kuhusiana na walengwa kadhaa kuzitumia fedha hizo kunywea pombe badala ya kuzitumia kwa mambo ya msingi yaliyokusudiwa. Matukio mengine ni baadhi ya walengwa kubainika kuwa na uwezo wa kujikimu kimaisha, hivyo kukosa sifa za kuendelea kunufaika na mpango huo.
Tasaf imekuwa ikiziondoa baadhi ya kaya maskini katika mpango huo kutokana na kasoro hizo pamoja na kaya ambazo walengwa wake wamefariki na wengine kuhama maeneo yao.
Kutokana na kasi ya matukio haya, tunaona kuwa kuna kasoro ambazo uongozi wa Tasaf haunabudi kuzifanyia kazi ili mpango huo uendelee kutekelezwa na kuwanufaisha walengwa halisi.
Baadhi ya mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi ni suala la tathnini ya kuzitambua kaya maskini. Tunashauri kwamba ifanyike tathmini ya kina ya kuzitambua kaya ambazo kweli ni maskini na Tasaf ijiridhishe bila kuacha shaka yoyote.
Tunasema hivyo kutokana na baadhi ya kaya zenye uwezo wa kipato kutumia udhaifu uliopo kuorodheshwa, tena kuna malalamiko kuwa kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia nafasi zao kujiorodhesha.
Kadhalika, kuna haja kwa Tasaf kuendelea kutoa elimu kwa walengwa wa mpango huo kuhusiana na matumizi ya fedha hizo; kwamba ni kwa ajili ya kuwasaidia kwa ajili ya mambo ya msingi na siyo starehe, ikiwamo kuzinywea pombe.
Aidha, itakuwa vizuri kwa Mfuko huo kuweka vizuri kumbukumbu sahihi za walengwa wa mpango huo na kuwafuatilia kwa karibu ili wanapofariki au kuhama maeneo husika wanaondolewe katika mpango huo ili kuokoa fedha za umma na kuwakosesha fursa wahitaji wengine.
Tunaamini kuwa pamoja na changamoto zinazojitokeza, Tasaf ikiweka utaratibu mzuri wa kuzitambua kaya maskini na kuzifuatilia kwa karibu, mpango huo utakuwa na tija, ufanisi na kukidhi lengo lake la kuzinusuru kaya maskini.










