Ratiba Ligi Kuu msimu ujao izingatie uhalisia wa mahitaji, siyo mazoea

20Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ratiba Ligi Kuu msimu ujao izingatie uhalisia wa mahitaji, siyo mazoea

KWA muda mrefu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limekuwa kitovu cha lawama kutoka kwa mashabiki wa soka na wadau wengine wa mchezo huo kwa namna linavyosimamia na kuendesha Ligi Kuu Bara.

Pamoja na TFF kulalamikiwa katika maeneo mengi kuhusiana na usimamizi wa ligi hiyo, lakini eneo ambalo kila mwaka limekuwa msingi wa lawama ni upangaji wa ratiba za michuano hiyo.

Ligi Kuu Bara ilimalizika Mei 22 mwaka huu na Yanga kutwaa taji hilo, lakini nyuma yake, msimu huo umeacha lawama nyingi dhidi ya TFF.

Tulitegemea pengine kutokana na malalamiko mengi ambayo TFF imekuwa ikiyapata kila msimu, ingeweza kujirekebisha. Hata hivyo, inaonekana kama vile TFF imekuwa mtumwa wa kubeba lawama hata zile ambazo wangeweza kuziepuka.

Upangaji ovyo wa ratiba usiozingatia mahitaji ya kalenda za michuano ya kimataifa kwa klabu na timu za taifa, unaitesa TFF kila mwaka.

Tunashindwa kuelewa kama kweli TFF ina upeo unaohitajika katika kupanga ratiba za mechi za ligi kuu ili zisiingiliane na zile za michuano ya kimataifa.

Wakati huu wadau wa soka na mashabiki wakijiandaa kuona ratiba mpya ya msimu wa mwaka 2016/2017, bado kuna shaka kama kweli ratiba hiyo inaweza kukidhia mahitaji husika na kuiepusha na lawama zilizozoeleka kusikika kila msimu.

Nipashe, kama wapenda michezo, tunaamini TFF inaweza kupanga vizuri ratiba ya mechi za ligi kuu na kuiepusha ratiba hiyo kuingiliana na ratiba za michuano mingine.

Lakini hilo litawezekana tu iwapo TFF itakubali kuondokana na utumwa wa kuwa kiini cha lawama kila msimu.

Kukubali kuondokana na utumwa huo, ina maana shirikisho hilo lazima sasa lije na mikakati mipya ya kupanga ratiba kwa kuzingatia uhalisi na siyo kufanya kwa mazoea.

Kuna mifano mingi TFF inaweza kujifunza namna ya kuepukana na lawama za upangaji mbovu wa ratiba za mechi za Ligi Kuu.

Kwa mfano, tayari ratiba ya mechi za Ligi Kuu England imeshapangwa mapema katika utaratibu uliozingatia zaidi kalenda ya kimataifa.

Ni vigumu kwa Ligi Kuu England kukuta mechi zake zikiingiliana na ratiba za mechi za kimataifa.

Kwanini TFF isisimame kwenye mstari wa uhalisia na kuondokana na lawama zilizo ndani ya uwezo wao?
Nipashe tunaishauri TFF kubadilika na kufanya mambo kulingana na mahitaji na uhalisia na siyo tena kufanya kazi kwa mazoea.

Tumechukua fursa hii mapema kuishauri TFF kuwa makini katika upangaji wa ratiba za mechi za ligi kuu msimu ujao ili kuepusha wadau kutisha shaka juu ya uwezo na utendaji wa viongozi wao.

Tungependa kuona msimu ujao unakuwa mfano wa pekee na aina yake katika upangaji wa ratiba.

Ratiba ya msimu ujao iwe na tija badala ya lawama. Iwe msingi wa kuepusha lawama na manung’uniko kama ilivyokuwa msimu uliomalizika.

Kama TFF itafanikiwa kufanya hayo, Nipashe tuna uhakika ligi ya msimu ujao itabeba ushindani mkubwa itakaowaepuesha mashabiki kupoteza muda wao kulalamikia upangaji ovyo wa ratiba ya mechi za Ligi Kuu.