Uzimaji wa simu bandia uwe fundisho kwa wote

17Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Uzimaji wa simu bandia uwe fundisho kwa wote

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jana usiku ilizizima simu zote bandia za mikononi zilizokuwa zinatumiwa na wateja wa kampuni kadhaa za simu.

Simu hizo zilizimwa baada ya muda uliotolewa na mamlaka hiyo kwa wamiliki wa simu hizo kununua simu halisi ili kuepukana na usumbufu ambao ungewapata kutokana na simu zao kuzimwa.

Kabla ya hapo Serikali pamoja na TCRA walitoa maelezo ya kina kuhusiana na uamuzi wa kuzizima simu bandia. Miongoni mwa sababu hizo ni madhara mbalimbali yatokanayo na simu hizo yakiwamo ya kiafya na Serikali kupoteza mapato mengi kutokana na uingizwaji wa simu hizo bila kulipa kodi.

Ingawa watumiaji wengi wa simu hizo awali walipinga uamuzi wa kuzimwa kwa simu hizo kwa kutoa sababu kadhaa, lakini kadiri Serikali ilivyozidi kusisitiza kuwa haitabatilisha uamuzi huo, watu hao walibadilika na kukubaliana na uamuzi huo.

Uamuzi wa Serikali wa kuzizima simu bandia inawezekana ukawa umewaathiri baadhi ya waliokuwa wanazitumia, lakini tunapaswa kukubaliana na hatua hiyo kutokana na uzito wa sababu zilizoelezwa na Serikali.

Suala la afya ni muhimu kwa kila binadamu, hivyo kama wataalamu wa afya wamebaini kuwa simu hizo zina madhara kwa afya, basi hapakuwapo sababu ya kuendelea kuzitumia. Kadhalika, taarifa kwamba simu hizo zilikuwa zinaingizwa nchini bila kulipiwa kodi, hivyo kuikosesha Serikali mapato zinamshawishi kila Mtanzania mzalendo akubaliane na uamuzi wa kuzifunga.

Ni kitu kisichokubalika kuwaacha watu wachache kuingiza bidhaa zisizo na viwango na vilevile kuinyima Serikali mapato yake, ambayo yangetumika kuiendesha pamoja na kutoa huduma muhimu kwa wananchi.

Tunaamini kuwa uamuzi wa Serikali kuzizima simu bandia utakuwa fundisho kwa wananchi kujiepusha kununua bidhaa zisizo na viwango. Ni matumaini yetu kuwa wengi wamefunguka macho na kwamba kuanzia sasa watajenga utamaduni wa kununua simu zinazoendana na viwango vya TCRA pamoja na bidhaa nyingine zinazokidhi viwango vya Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Tunatoa angalizo hilo kwa kuwa idadi kubwa ya Watanzania wanaotumia huduma za simu za mkononi inaongezeka kwa kasi kubwa kila uchao kwa sababu ya kupatikana kwa urahisi na bei nafuu kwa simu na vifaa vyake.

Sababu kubwa ambayo tunadhani ilichangia ongezeko kubwa la matumizi ya simu bandia ni mamlaka zetu kukosa umakini kutokana na kutokuweka taratibu za kufuatilia uingizwaji wake kutoka nje ya nchi.

Kwa kuwa suala zima la ufuatiliaji ni mtambuka; kwa maana ya kuzishirikisha mamlaka mbalimbali kama TCRA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), TBS na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, zote kwa pamoja hazikutimiza wajibu wao kama zinavyopaswa.

Kwa mfano Wizara na TCRA kama wasimamizi wa sera, walipaswa kuchukua hatua mapema. Kwa upande wake TRA ilipaswa kuhakikisha walioingiza simu hizo wanazilipia kodi ya Serikali wakati TBS ilipaswa kuzikagua simu hizo kuhakikisha kwamba zinakidhi viwango vya ubora, vinginevyo kuzikamata na kuziharibu.

Njia pekee ambayo tunadhani inaweza kudhibiti uingizaji wa bidhaa bandia na zisizokidhi viwango, ni kuzikagua zikiwa katika nchi zinakotoka kabla ya kuruhusiwa kuingizwa nchini. Kutokana na hali hiyo, kuna haja kwa TBS kuweka utaratibu huo kama ambavyo imekuwa ikiyakagua magari yaliyotumika nje ya nchi kabla ya kuingizwa nchini.