Maadhimisho haya hufanywa Juni 16 kila mwaka tangu ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (sasa Umoja wa Afrika).
Uamuzi wa kuanzisha maadhimisho hayo unatokana na tukio la mauaji ya risasi yaliyofanywa na askari wa utawala wa ubaguzi wa rangi wa Makaburu dhidi ya mamia ya watoto weusi huko Soweto, Afrika Kusini, waliokuwa wakiandamana mitaani kupinga kulazimisha kufundishwa kwa lugha ya kiafrika na mazingira mabaya ya shule za weusi.
Wakati tunaadhimisha kumbukumbu hiyo leo, tunapswa kuzingatia kwamba jamii nzima inawajibika kuwapa watoto haki zao za msingi sambamba na kuwalinda dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili vinavyofanana na tukio la kinyama la mauaji ya Soweto.
Licha ya tukio la ukatili wa mauaji ya Soweto dhidi ya watoto ambao hawakuwa na hatia zaidi ya kudai haki yao ya msingi ya kupata elimu bora, watoto wa Afrika wanaendelea kufanyiwa vitendo va ukatili na udhalilishaji vya kulawitiwa, kubakwa, ukeketaji wa watoto wa kike, kinyimwa fursa za elimu, ajira mbaya, mimba za utotoni, ndoa za utotoni pamoja na kutelekezwa na wazazi, hivyo kusosa matunzo na matokeo yake kuwa watoto wa mitaani.
Licha ya asasi kadhaa kuelekeza jitihada katika utetezi wa haki za watoto, kila uchao zinaibuka changamoto mpya dhidi ya watoto ambazo zijaifanya jamii kuendelea kwa na wajibu wa kukabiliana nazo kwa lengo la kuwalinda watoto.
Miradi kadhaa kama wa Mpango wa Kutokomeza Ukatili na Unyanyasaji wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto (Gewe ll) unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) na mingine hainabudi kuwa endelevu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba pamoja na mambo mengine, hali za watoto zinaendelea kulindwa.
Jitihada hizo za kuibua, kufuatilia na kuchukua hatua kuhusu matukio ya udhalilishaji na ukatili dhidi ya watoto zinapaswa kuungwa mkono na Serikali kwa kusimamia na kutekeleza sheria zilizoko na ikiwezekana zitungwe sheria mpya pale inapobainika kuwa zilizoko zimepitwa na mazingira halisi ya sasa.
Kwa mfano, kuna sheria inayowabana wazazi wasiotimiza wajibu wao wa kuwalea watoto na kuwapatia mahitaji ya msingi. Kadhalika, kuna sheria inayotoa adhabu dhidi ya watu wanaowafanyia watoto vitendo vya udhalilishaji na ukatili hususani ubakaji, kulawiti, mimba za utotoni na kuwaoa watoto ambao hawajafikisha miaka 18.
Hata hivyo, utekelezaji wa sheria hizi umekuwa ndogo na matokeo yake kasi ya vitendo hivyo inazidi kuongezeka kila uchao. Kutokana na hali hiyo, tunaikumbusha jamii kuchukua hatua za haraka ikiwamo kuishinikiza Serikali kuwa makini kuzitekeleza sheria hizo na kutungwa sheria mpya ambazo zinakidhi mazingira ya sasa ambayo watoto wanahitaji kupewa ulinzi wa uhakika.
Kwa kuwa watoto waliouawa Soweto walikuwa wanadai haki ya kupata elimu bora katika mazingira bora, tunashauri kwamba Serikali za nchi za Afrika zihakikishe kwamba watoto wote wanapewa fursa
ya kupata elimu bora kwa ajili ya kuwajengea msingi wa maisha yao ya baadaye.
Kwa Tanzania, hatua ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutoa elimu bure tunaamini kuwa itawawezesha watoto wengi kusoma elimu ya msingi na sekondari, hivyo kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili watoto.










