Kambi ya Yanga Uturuki izae matunda

13Jun 2016
Mhariri
Nipashe
Kambi ya Yanga Uturuki izae matunda

YANGA wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, wako nchini Uturuki kujiandaa na mashindano hayo hatua ya makundi.

Mabingwa hao wa Bara, wamepangwa Kundi A pamoja na Mo Bejaia ya Algeria, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Medeama ya Ghana.

Katika kampeni hiyo, Yanga itaanza ugenini Juni 17 kwa kucheza dhidi ya wapinzani wao wa Algeria, Mo Bejaia, kabla ya kurudi nyumbani kucheza dhidi ya TP Mazembe ya DRC.

Nipashe tunaamini, uamuzi wa Yanga kwenda kupiga kambi nje ya nchi umelenga kuiandaa timu hiyo kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ambayo huwa na ushindani mkubwa kutokana na kuzijumuisha klabu kubwa barani na zenye ushindani mkubwa.

Tunatambua gharama kubwa walioingia Yanga kwenda kupiga kambi nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi hayo, lakini haliwezi kuwa tatizo kama timu itafanya vizuri kwenye mashindano.

Tungependa kuchukua nafasi hii kuwakumbusha wachezaji wa Yanga kuwa safari yao ya kwenda kujiandaa nje ya nchi, siyo sawa na utalii, bali ni kwenda kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na washindani wao.

Kama alivyosema Kocha Hans van de Pluijm kuwa wanakwenda kuiandaa timu kushiriki na siyo kusindikiza, ndivyo wote tungependa kuona kauli hiyo inatimia. Kwamba wachezaji walitambue hilo na kufanya maziezi kwa kujituma wakitambua kuwa wao ni wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

Pluijm amezungumza kama kocha, lakini jukumu kubwa linabaki kwa wachezajihao kusikiliza maelekezo ya benchi lao la ufundi. Wachezaji hao ndiyo kiini cha kuleta mafanikio.

Tunatambua kuwa timu inayojiandaa vizuri ndiyo inayokuwa jirani na mafanikio, hivyo basi tuna kila sababu ya kuamini kuwa maandalizi ya Yanga nje ya nchi yataleta matunda.

Wachezaji wa Yanga lazima watambue kuwa, michuano hii ni mikubwa kwa vile inazikutanisha timu zilizofanya vizuri.
Lakini pia nafasi ya Yanga kucheza michuano hiyo ni sehemu ya kujitangaza kimataifa kwa wachezaji wake. Yaani ni sehemu ya kujiuza kwa vilabu vya nje katika siku za baadaye.

Hivyo, basi tunawakumbusha kwa mara nyingine tena wachezaji kuwa makini na kufuata vizuri maelekezo watakayopewa na walimu wao pamoja na kuonyesha nidamu ya hali ya juu kwa makocha na viongozi watakaoongozana nao.

Tungependa kuona Yanga inafika mbali kwenye michuano hii na siyo kuwa sehemu ya wasindikizaji na kuwaacha wengine wakosonga mbele.

Viongozi walioambatana na timu nao wawe mstari wa mbele kuhakikisha wachezaji wanapata hudumu muhimu za kuwawezesha kuwa fiti kiakili na utajari wa kucheza kwa dhamira ya kupata matokeo mazuri.

Ingawa kwenye ushindani kuna kushinda, kufungwa au kwenda sare, lakini dhamira sahihi ya Yanga kwenye mashindano hayo ibaki moja tu, nayo ni ushindi kila mchezo.

Kadhalika, wachezaji na viongozi hao wanapaswa kujiandaa wakielewa kuwa katika muchuano hiyo, vilabu vinavyoshiriki hutumia mbinu mbalimbali za kupata ushindi zikiwamo za ndani na nje ya uwanja, hivyo, tunawashauri kwamba maandalizi yao yafanyike huku nao wakiwa na mikakati ya kukabiliana na mbinu hizo.