Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Kinga katika Wizara ya Afya Zanzibar, Dk. Mohamed Dahoma juzi ilisema Wafanyakazi wanatakiwa kupunguza nywele, masharubu na ndevu wakiwa katika maeneo yao ya kazi.
Dk. Dahoma alisema pia miongoni mwa masharti mengine kadhaa, wafanyakazi watatakiwa kupima afya zao kila baada ya miezi sita.
Ukiacha masharti ya afya katika ngazi ya wahudumu, Wizara pia imetaka kila mgahawa uwe na bomba la kutolea moshi juu lenye urefu usiopungua futi 10 pamoja na vyoo viwili, kwa matumizi ya wanawake na wanaume.
Aidha, Mkurugenzi wa Kinga katika Wizara ya Afya Zanzibar huyo alisema wamiliki wa migahawa ni lazima wazingatie usafi, ikiwemo chakula kuhifadhiwa katika vyombo maalum bila ya kufikiwa na wadudu na maji ya kunawa kuwa ya moto.
Licha ya kuwa taarifa hii ya Wizara ya Afya Zanzibar imekuja katika kipindi ambacho visiwa hivyo vina mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, na masharti hayo kuwa na lengo la kudhibiti maradhi hayo, tuna wasiwasi, Nipashe, kwamba yanaweza kuonekana kuwa kero kwa waendesha migahawa Wazanzibari wengi.
Tuna wasiwasi huo Nipashe, kwa sababu kimsingi wenyeji wa visiwa hivyo ni watu wenye kushika sana tamaduni kulinganisha na makabila mengi nchini.
Kwenye usafi wa mwili kwa mfano, tunafahamu Nipashe, itakuwa si rahisi sana kwa Mzanzibari mwenye mapenzi ya kufuga ndevu, kwa mfano, kukubali kunyoa ndevu na kubaki na kidevu kinachong'aa mafuta.
Aidha, linapokuja suala la kunyoa sharubu, kwa mfano pia, itakuwa si rahisi kwa ustaadhi wengi kukubali kunyoa nywele hizo za juu ya mdomo kwa sababu tu ni moja ya mashari ya kufanya kazi ya uhudumu kwenye mgahawa.
Zanzibar, aidha, haiwezi kuwa Zanzibar bila ya 'vijiwe' vinavyouaza chips katika maeneo ya wazi, katika maeneo mbalimbali ya kuzunguka Mji Mkongwe, achilia mbali Forodhani; hasa nyakati za usiku.
Lakini Serikali inapokuja na utaratibu tofauti na maisha ya kila siku ya Mzanzibari sasa, Nipashe tunaona, itakuwa ni makosa kama wakazi wa mji huo wataona ama ni bugudha, ama ni gharama ambazo hawawezi kuzimudu.
Ni imani yetu, Nipashe, kwamba hakuna gharama inayoweza kutosha bei ya uhai wa binadamu; Wazanzibari wenyewe wakiwemo.
Hivyo tuchukue nafasi hii, basi, Nipashe, kuwaomba Wazanzibari wote kupokea masharti mapya haya yanayoongoza biashara ya migahawa kwa mikono miwili ili nchi kwa ujumla ifanikiwe kutokomeza kipindupindu ambacho kimsingi, ni zao la uchafu.










