Fabregas: Haiwezekani kurudi Barcelona

15May 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Fabregas: Haiwezekani kurudi Barcelona

KIUNGO wa Chelsea, Cesc Fabregas (29), amesema kwa sasa hawezi tena kurejea kwenye klabu yake ya zamani ya Barcelona ingawa anatamani iwe hivyo.

Cesc Fabregas

Nyota huyo, alisema kuwa nafasi na wakati wake wa yeye kucheza kwenye kikosi cha mabingwa hao wa Hispania umeshapita na ni jambo gumu kurejea tena Camp Nou.

"Kurudi Barcelona ni kitu ambacho hakiwezekani tena ingawa ni jambo ambalo ningependa litokee," Fabregas alisema.
Nahodha huyo wa zamani wa Arsenal, alijiunga na Barcelona mwaka 2011 na kuichezea timu hiyo kwa miaka mitatu akitwaa ubingwa wa La liga kabla ya kurejea Ligi Kuu England akiwa na Chelsea.

Alisema atabaki Chelsea na anajiandaa kwa msimu mpya chini ya kocha mpya, Antonie Conte ambapo anaamini mambo yataenda vizuri na kusahau jinamizi la mwanzo mbaya kwenye ligi msimu huu.

"Tulianza vibaya msimu huu, maandalizi hayakuwa mazuri na baadhi ya wachezaji hawakuwa kwenye ubora wao, tumebadilika mwishoni lakini naamini tutakuwa na mwanzo mzuri msimu ujao tukiwa na kocha mpya," alisema Fabregas.

Akizungumzia ujio wa kocha huyo mpya, nyota huyo alisema kuwa, kocha huyo wa zamani wa Juventus ni mpambanaji na ni kocha mkubwa.

"Anajua nini anachofanya na ametwaa makombe na klabu kubwa, najiandaa kuanza msimu mpya na yeye nikitegemea kujifunza mengi kutoka kwake," alisema Fabregas.