Chembe hizi au seli ndizo huunda misuli na viungo vingine vingi mwilini. Pia ni chanzo kikuu cha nishati ubongoni.Zipo aina kuu mbili za kisukari nazo ni ‘type one’ na ‘type 2’. Kwa nyakati nyingine, mwili huweza kuwa na kiwango kikubwa cha sukari kuliko kawaida japo hali hiyo haiwezi kutafsiriwa kwamba ni kisukari.
Sukari kuzidi ndani ya damu huweza pia kuwapata wajawazito japokuwa hali hutengamaa baada ya kujifungua.
‘Type 1 hujitokeza kwa watoto wadogo japo huweza kuonekana wakati wowote.
Wakati ‘type 2’ hutokea mara nyingi zaidi kwa watu wazima lakini inaweza kujitokeza katika umri wowote.
DALILI
Hutofautiana kulingana na kiwango cha sukari iliyozidi kwenye damu. Kwa ‘type 1’ dalili hutokea haraka na huwa hatari zaidi ya aina ya pili ‘type 2’ ambayo mgonjwa anaweza asizione mapema.
Dalili zake ni pamoja na kuhisi kiu mara kwa mara, kukojoa sana, kuhisi njaa isivyo kawaida, kupoteza uzito, uchovu wa mara kwa mara, kuhisi kukosa nguvu, kuwa na uoni hafifu, vidonda kuchukua muda mrefu kupona, kupata mashambulizi au maambukizi ya mara kwa mara mdomoni, ngozi na sehemu za siri.
CHANZO
Tuanze kuangalia Insulini ambayo ni homoni inayozalishwa katika kongosho (pancrease) na kazi yake ni kurekebisha kiwango cha sukari ‘glukosi’ kwenye damu kwa kusaidia uchukuliwaji wa sukari kutoka kwenye damu kwenda kwenye misuli na sehemu nyingine kuhifadhiwa.
KAZI YA INSULIN
Kongosho huzalisha insulin na kuimwaga kwenye mishipa ya damu ili kuanza uchukuliwaji wa sukari kutoka kwenye damu kwenda kwenye chembe hai za mwili hivyo husaidia kurekebisha kiwango cha sukari kwenye damu.
Kadri kiwango cha sukari kwenye damu kinavyopungua ndivyo hivyo uzalishaji wa insulin hupungua.
KAZI YA SUKARI
Hiki ni chanzo kikuu cha nguvu mwilini ‘glukosi’ hupatikana kutoka kwenye vyanzo vikuu viwili; chakula na ini. Sukari hutolewa kwenye damu na kuingia kwenye chembe hai kwa msaada wa homoni ya insulin.Ini huhifadhi na huzalisha sukari.
Wakati kiwango cha sukari mwili ni kidogo kama mfano ukiwa na njaa, ini huvunjavunja aina nyingine ya sukari iitwayo ‘glycogen’ na kuibadili kuwa glukosi ili kusaidia kuweka kiwango cha sukari mwilini kwenye uwiano wa kawaida.
CHANZO TYPE 1
Hadi sasa hakijulikani. Kinachofahamika ni kuwa kinga ya mwili ambayo husaidia kuharibu vimelea na virusi wavamizi hushambulia na kuharibu chembe hai za kongosho zinazozalisha insulin.
Hii husababisha mwili kuwa na kiwango kidogo au kutokuwa na insulin na kusababisha sukari kuzidi kwenye damu kwani hisafirishwi mwilini. Aina hii ya kisukari husababishwa na kurithiwa.
CHANZO TYPE 2
Aina hii hutokea ikiwa mwili umeshindwa kuzalisha insulin ya kutosha au chembe hai za mwili zinaposhindwa kufanya kazi na insulin iliyopo. Hii ina maana kuwa sukari ‘glukosi’ itaendelea kubaki kwenye damu na hivyo haitatumika kwa kazi ya kuzalisha nguvu. Chanzo kamili cha tatizo hili hakijulikani japo masuala ya kurithi na mazingira huchangia.
Kunenepa kupindukia kunasadikiwa pia kuwa chanzo cha aina hii ya kisukari japo si watu wote wenye kisukari ni wanene kupita kiasi.
UKIWA MJAUZITO
Wakati wa ujauzito, mwili huzalisha homoni mbalimbali kama oestrogen, progesterone na human placental lactogen (HPL) ambazo uwepo wake kwa wingi mwilini husababisha usugu kwa chembe hai dhidi ya homoni ya insulin na hivyo kusababisha chembe hai kushindwa kushirikiana vizuri na insulin kupokea sukari kutoka kwenye damu.
Inasababisha sukari kushindwa kupokelewa na chembe hai hizi na hivyo kiwango cha sukari kwenye damu kuwa kikubwa. Usugu wa chembe hai za mama kushindwa kupokea glokosi ni ili kusaidia kiwango cha kutosha cha sukari ‘glukosi’ kielekezwe kwenye kiumbe aliye tumboni ili akue vizuri.
VISABABISHI TYPE 1
Ni pamoja na historia ya familia iwapo mzazi au ndugu wa kuzaliwa aliwahi kuugua kisukari aina hii.
Uharibifu wa kinga mwilini hutokea kwa wanaougua ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza iwapo walishambuliwa na kuharibiwa kinga ya mwili.
TYPE 2
Uzito mkubwa, wingi wa mafuta mwilini husababisha chembe hai za mwili kushindwa kushirikiana na homoni ya insulin kupokea sukari ndani ya damu.
Kutofanya mazoezi, kiasi unavyozidi kuwa mvivu ndivyo hatari ya kupata aina hii ya kisukari.Mazoezi husaidia kupunguza uzito na kusaidia matumizi ya sukari mwilini na hivyo kuzifanya chembe hai kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi na homoni ya insulin.
Historia ya familia endapo mzazi mmojawapo au ndugu wa kuzaliwa tumbo anapokuwa na aina hii ya pili ya kisukari unaweza kurithiwa.
Umri hatari ya kuugua ugonjwa huu huongezeka kadiri unavyokuwa mkubwa. Pengine ni kutokana na uwezo mdogo wa kufanya mazoezi ya mwili.
Presha ya kupanda, kwa mtu mwenye presha kubwa zaidi ya ‘140/90 mmHg’ yupo kwenye hatari kubwa ya kupata kisukari aina ya pili.
Kwenye ujauzito- Iwapo mtu amewahi kupata kisukari wakati wa ujauzito ana uwezekano wa kuwa na aina ya pili.


.jpg?itok=nfwjwDzv)








