Kuipa ushindi Yanga kutokana na vurugu zilizotokea kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani na kusababisha mchezo kuvunjika huku, Yanga ikiwa mbele kwa magoli 2-1.
Nipashe, tunaamini kamati hiyo ilijiridhisha na ripoti ya kamisaa wa mchezo na kuamua kuipa ushindi Yanga kwa kufuata kanuni.
Kamati imeilima Coastal Union Sh. milioni 2 kama faini kwa mashabiki wake kufanya vurugu, lakini pia imemfungia mwaka mmoja mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo, Abdallah Kambuzi.
Vurugu za Mkwakwani zimeacha doa ambalo TFF na wadau wengine wanapaswa kulifuta kwa kuhakikisha matukio kama hayo hayapewi nafasi tena.
Katika zama hizi, ni aibu kwa mashabiki kufanya fujo uwanjani na kusababisha mechi kuvunjika kama kilelezo cha kutokubaliana na uamuzi wa refa.
Kitendo hiki kimetia aibu soka la Tanzania, lakini pia kimetoa picha mbaya kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Vitendo kama hivyo vinapaswa kukemewa kwa nguvu kubwa, ikiwa ni pamoja na wahusika kutiwa nguvuni na kufunguliwa mashtaka.
Ni kwa sababu, soka ni mchezo wa furaha, hivyo inapojitokeza mashabiki wachache wanaugeuza kuwa vurugu, maana yake ni kuharibu taswira na utamaduni wa Kitanzania, lakini pia kwenda kinyume na sheria zinazoratibu mchezo huo.
Tunapougeuza mchezo wa soka kuwa sehemu ya vurugu badala ya burudani, maana yake tunafungua milango ya wadhamini wachache tuliona kutukimbia.
Tumaamini, hakuna mdhamini atakayekuwa tayari kuwekeza fedha zake kwenye mchezo ambao badala kujenga ushindani wa kweli, unakuwa sehemu ya vurugu.
Hivyo, tungependa kuona zilizotolewa kwa wahusika wa vurugu za Mkwakwani zinakuwa fundisho kwa watu wengine.
Lakini pia katika kuweka msisitizo, tungependa kuishauri TFF kufanya kazi kwa karibu na Jeshi la Polisi ili kuwakamata watu watakaobainika kufanya fujo na kufunguliwa mashtaka, tukiamini kuwa kuiadhibu klabu peke yake hakuwezi kuwa suluhisho la kudumu.
Katika hali hiyohiyo, tunapenda kuweka msisitzo kwa viongozi wa klabu kuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa mashabiki wao.
Tunapenda pia kuwaomba mashabiki wachache wenye utamaduni wa kufanya vurugu uwanjani kuacha tabia hiyo mara moja.
Mashabiki lazima wajifunze uvumilivu hasa timu zao zinapofungwa, lakini pia lazima waelewe kuwa kwenye ushindani kuna kushinda, kushindwa na kwenda sare.
Matokeo haya yawe tayari kukubaliwa na mashabiki hata kama kuna makosa ya kibinadamu yamefanyika na kusababisha timu zao kushindwa.
Tungependa kuona soka letu linakuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine, lakini hilo linaweza kuepukika tu kwa kusimama kwenye maadili mengi, nidhamu na kufuata sheria na kanuni za mchezo wa soka.










